1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel yaruhusu misaada ya kiutu kuingia Gaza

Sylvia Mwehozi
19 Oktoba 2023

Israel imetangaza kwamba itaruhusu misaada ya kiutu kuingia Ukanda wa Gaza kutokea nchi jirani ya Misri, wakati ikiendelea na mzingiro wake katika eneo hilo la Wapalestina tangu shambulio baya la wanamgambo wa Hamas.

Misafara ya malori ikisubiri kuelekea Gaza
Msafara wa malori yaliyosheheni misaada ya kibinadamu kutokea Misri ukisubiri kupewa ruhusa ya kupita kivuko cha Rafah tayari kuelekea GazaPicha: REUTERS

Ofisi ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema katika taarifa yake baada ya uamuzi wa baraza la mawaziri kwamba "kutokana na maombi ya Rais wa Marekani Joe Biden, Israel haitozuia usambazaji wa misaada ya kiutu kupitia Misri".

Taarifa hiyo hata hivyo imesisitiza kwamba misaada ya kiutu kwa raia walioko kusini mwa Gaza itaruhusiwa tu "endapo haitolifikia kundi la Hamas" ambalo linatawala eneo hilo. Mkurugenzi wa Shirika la afya duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amekaribisha tangazo hilo na kusema kwamba "maisha ya watu wengi yanategemea uamuzi huo".

Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Tel AvivPicha: Avi Ohayon/Israel GpoI/Zuma/MAGO

Raia wa Gaza wamekabiliwa na uhaba mkubwa wa mahitaji ya msingi baada ya eneo hilo kuzingirwa kufuatia shambulizi la kushtukiza la Hamas dhidi ya Israel, ambamo Waisraeli wapatao 1400 waliuawa na maelfu kujeruhiwa.

Shambulizi la Hospitali: Watu 500 waripotiwa kuuawa Gaza kwenye shambulio hospitalini

Wakati tangazo hilo likitolewa, Rais Joe Biden amekamilisha ziara yake ambayo ameitumia kutangaza msaada wa Dola milioni 100 kwa Wapalestina huko Gaza na Ukingo wa Magharibi. Akizungumza na waandishi wa habari, Biden amesema "watu wa Gaza wanahitaji chakula, maji, madawa na malazi".

Rais huyo amekiri kwamba misaada inayoingia Gaza itapekuliwa na haitopaswa kuwafikia Hamas, bila kutoa ufafanuzi ikiwa analenga tawi la wapiganaji, viongozi wa kisiasa au wizara za serikali zinazoendeshwa na kundi hilo. Wakati wa ziara yake Biden, pia ameahidi msaada wa kijeshi kwa Israel haswa katika kuhakikisha kwamba mfumo wake wa ulinzi wa angani Iron Dome unaendelea kufanya kazi.

Hapo jana pia, Marekani ilipinga azimio la Umoja wa Mataifa kulaani ghasia zote dhidi ya raia katika vita vya Israel na Hamas na kuhimiza msaada wa kibinadamu kwa Wapalestina huko Gaza, ikisema ni mapema mno kuandaa azimio mwafaka la Baraza la Usalama katika mgogoro huo.

Watu zaidi ya 500 wadaiwa kuuwawa hospitalini Gaza

01:49

This browser does not support the video element.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield alisema baraza hilo linahitaji kuruhusu juhudi za sasa za kidiplomasia na kutafuta ukweli zaidi wa kile kinachoendelea.

Balozi huyo pia alikosoa hatua za kushindwa kusisitiza haki ya Israel kujilinda. Azimio hilo lililoandaliwa na Brazil lilikuwa na uungwaji mkono mkubwa na lingelaani ghasia zote dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na "mashambulio mabaya ya Hamas" dhidi ya Israel.

Wakati huo huo uongozi wa Palestina umesema kuwa kitendo cha kuwahamisha raia kinguvu kutoka Ukanda wa Gazani kuvuka mstari mwekundu na haitoruhusu hilo kutokea. Taarifa hiyo imetolewa baada ya viongozi kukutana mjini Ramallah.

Katika hatua nyingine maelfu ya raia katika nchi za Kiarabu na Kiislamu duniani jana waliandamana kupinga vifo vya mamia ya watu katika shambulizi la hospitali mjini Gazana kuishutumu moja kwa moja Israel licha ya kwamba imekana kuhusika.

Israel na wanamgambo wa Hamas wametupiana lawama kwa shambulio hilo la hospitali, huku jeshi la Israel likisema baadaye lilikuwa na "ushahidi" kwamba wanamgambo walihusika.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW