Israel yaruhusu ujenzi wa makazi Ukingo wa Magharibi
3 Aprili 2017Baraza la mawaziri la Israel linaloshughuilikia masuala ya usalama kwa kauli moja hapo Alhamisi usiku limeunga mkono kile kinachooneka kama ni serikali ya mrengo mkali kabisa wa kulia kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Israel kuendelea na utanuzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi kwa kugaidi mashaka ya kimataifa juu ya suala hilo.
Kura ya kuunga mkono ujenzi wa makaazi mapya ya walowezi wa Kiyahudi katika eno linaloitwa Emek Shilo imekuja baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuwaambia waandishi wa habari kwamba wametowa ahadi wataanzisha makazi mapya ya walowezi na ahadi hiyo walikuwa wanaitimiza hapo jana.
Afisa mwandamizi wa Wapalestina Hanan Ashrawi amesema hatua hiyo inaonyesha kwamba serikali hiyo ya Israel inaendelea na sera zake za ukoloni wa walowezi, utawala wa ubaguzi wa rangi , kutokomeza kizazi na kupuuza kabisa haki za binaadamu za Wapalestina.
Umoja wa Mataifa pia yalaani
Amesema Israel imejitolea zaidi katika kuwatafadhalisha wananchi wake walowezi kinyume na sheria badala ya kutimiza mahitaji ya utulivu na amani ya haki.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antoni Guterres ameelezea kukatishwa tamaa na wasi wasi wa Katibu Mkuu huyo kufuatia tangazo hilo.Spephanie Dujarric amesema katika taarifa kwamba katibu kuu huyo amekuwa akisisitiza kwamba hakuna mpango B kwa Wapalestina na Waisrael kuishi pamoja kwa amani na usalama na analaani hatua zote za upande mmoja kama hiyo ya sasa ambayo inatishia amani na kuyumbisha suluhisho la kuwepo kwa mataifa mawili.
Tangazo hilo la Israel pia limekuja wakati Wapalestina wakiadhimisha miaka 41 ya Siku ya Ardhi katika Ukanda wa Gaza hapo Alhamisi. Miongoni waliozungumza katika maadhimisho hayo ni pamoja na Ismail Radwan kiongiozi wa kundi la Hamas ambaye amesema "Tunatuma ujumbe kwa mataifa ya Kiarabu na mataifa ya Kiislamu ni muhimu kuunga mkono msimamo thabiti wa wananchi wa Palestina Ujumbe wetu kwa wale wanaoikalia ardhi yetu kwa mabavu, kukaliwa huko kwa radhi yetu kwa mabavu kutakoma haki haziwezi kuachwa kudaiwa kutokana na kupitwa na wakati au kwa kukaliwa kwa mabavu na ardhi yetu haiwezi kugawiwa ni kwa ajili ya watu wetu."
Hakuna taarifa kutoka Marekani
Hakukuwa na taarifa iliyotolewa mara moja kutoka utawala wa Rais Dobnald Trump wa Marekani ambao uko katika mazungumzo na Israel juu ya kuweka kikomo kwa ujenzi wa makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ambayo Wapalestina wanataka kuunda taifa lao.
Makazi hayo katika ardhi ambayo Israel iliiteka katika vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967 yanachukuliwa kuwa sio halali takriban na dunia nzima.
Israel inayataja kwamba ina husiano wa kibiblia,kihistoria, kisiasa halikadhalika maslahi yake ya usalama kwa ardhi hiyo.
Mwandishi : Mohamed Dahman / Reuters/AFP
Mwandishi :Mohammed Abdul-Rahman