Israel yasema Iran yaandaa mashambulizi ya kulipiza kisasi
12 Agosti 2024Majeshi ya Israel yanaendelea na operesheni yake karibu na eneo la kusini mwa Gaza katika mji wa Khan Younis hii leo Jumatatu huku jamii ya kimataifa ikiendelea kuweka msukumo wa kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza ili kuepusha vita hivyo kulitumbukiza eneo la Mashariki ya Kati katika mgogoro kati ya Israel na Iran na washirika wake.
Watu wapatao 142 wameuawa katika muda wa saa 48 zilizopita katika mashambulizi ya Israel. Madaktari wa Palestina wamesema kwenye mji wa Khan Younis leo Jumatatu watu wasiopungua 16 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa.
Soma Pia Israel yashutumiwa kwa mauaji ya halaiki baada ya shambulizi la shule moja mjini Gaza
Familia zaidi na watu waliokimbilia kwenye mji huo wanatakiwa waondoke kutoka kwenye eneo hilo kutokana na maagizo mapya yaliyotolewa na jeshi la Israel.
Wakati huo huo mashirika ya ndege yametangaza kuongeza muda wa kusimamisha safari za kwenda na kutoka katika nchi za Mashariki ya Kati huku eneo hilo likikabiliana na uwezekano wa Iran na Hezbollah kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi.
Mashirika ya ndege yasitisha safari
Shirika la ndege la Ujerumani, Lufthansa limesema safari zake zote za ndege kwenda na kutoka Tel Aviv, Tehran, Beirut, Amman na Erbil zimesimamishwa hadi Agosti 21. Shirika hilo limesema ndege zake pia hazitatumia anga za Iraq na Iran.
Lufthansa imesema mashirika ya ndege ya Swiss, Austrian, Brussels na Eurowings pia yamesitisha safari za ndege za abiria na za mizigo.
Shirika la ndege la Ufaransa nalo limechukua hatua kama hizo, limesimamisha safari zake kutoka Paris kwenda na kurudi Beirut kutokana na hali ya usalama nchini Lebanon.
Vilevile shirika la safari za ndege za bei ya chini la Ireland, Ryanair limesema limeahirisha safari zake zote za ndege kwenda na kutoka Tel Aviv.
Soma Pia: Hamas yataka utekelezaji wa mpango wa amani wa Biden Gaza
Kwingineko Makao makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican yametoa wito kwa Iran kujizuia kwa kila njia kuuchochea mzozo wa Mashariki ya Kati.
Waziri wa mambo ya nje wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, alipozungumza kwa simu na rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian aliisisitizia Iran kufuata njia ya mazungumzo na kuzingatia amani.
Kadinali Parolin alielezea wasiwasi mkubwa wa Vatican juu ya kinachotokea Mashariki ya Kati.
Hatua za kusitisha mapigano
Viongozi wa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza wameanzisha hatua za kushinikiza kusitishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza, kurejeshwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas na utoaji wa misaada kwa Wapalestina bila vikwazo.
Katika taarifa yao ya pamoja, viongozi hao kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, wamezitaka nchi wapatanishi Marekani, Qatar na Misri ziharakishe kupatikana makubaliano ya kumaliza vita kati ya Israel na kundi la Hamas.
Soma Pia: Shambulio la Israel kwenye shule huko Gaza lalaaniwa kimataifa
Pendekezo hilo ni la kuukubali mpango wa awamu tatu wa Rais wa Marekani Joe Biden ambapo Hamas watawaachilia mateka waliowachukua wakati wa shambulio la Oktoba 7 na Israel itawaachia wafungwa wa Kipalestina na kuyaondoa majeshi yake kutoka kwenye Ukanda wa Gaza.
Tamko la leo la viongozi hao watatu wa Ulaya pia limeitaka Iran na washirika wake kuepuka kufanya mashambulizi ambayo yatazidisha mivutano ya kikanda na kuhatarisha fursa ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kwa mateka kuachiliwa huru.
Vyanzo:AP/RTRE/DPA