Israel yashambulia barabara kuu ya Syria -Lebanon
10 Oktoba 2024Israel imeongeza mashambulizi yake nchini Syria tangu ilipofanya mashambulizi ya anga kwa kile ilichokisema inalengwa wanamgambo wa Hezbolllah wa Lebanon zaidi ya wiki mbili zilizopita, na hata kumuuwa kiongozi wake wa ngazi za juu.
Shirika la ufuatiliaji wa haki za binadamu la Syria lenye makao yake makuu nchini Uingereza limesema ndege za Israel zilifanya mkururo wa mashambulizi zikilenga barabara inayounganisha Syria na Lebanon katika eneo la Quseir upande wa Syria.
Rami Abdel Rahman Mkuu wa shirika hilo amesema mashambulizi hayo yalifanyika kama sehemu ya majaribio ya Israel "kukata mtandao wa usamabazi wa Hezbollah", na kuongeza kuwa hakuna majeruhi.
Soma pia:Hezbollah yadai kushambulia kambi ya jeshi ya Israel
Jeshi la Israel lilisema ndege zake zilishambulia maeneo ya wanamgambo wa Hezbollah karibu na mpaka.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch mapema wiki hii lilisema mashambulizi ya Israel karibu na mpaka wa Lebanon na Syria yanawaweka raia katika "hatari kubwa" kwani yaliwazuiwa kukimbia na kukwambisha shughuli za kiutu.
Kulingana na takwimu rasmi ongezeko la mashambulizi ya Israel dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon limesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200 na kuwalazimu wengine zaidi ya milioni moja kuyahama makazi yao. Zaidi ya watu laki nne wengi wao wakiwa ni Wasyria walikimbilia mpakani mwa Syria.
Israel yawauwa makamanda wengine wa Hezbollah
Jeshi la Israel limesema limewauwa makamanda wawili wa Hebzollah kusini mwa Lebanon, katika mashambulizi yake ya usiku kucha leo yaliolenga maeneo yanayochukuliwa kuwa ni ngome za Hezbollah na kushambulia maghala ya silaha.
Kituo cha habari cha Al Mayadeen chenye uhusiano na Hezbollah kilisema majengo ya makazi yalishambuliwa. Jeshi la Israel limeendelea kuwataka wakaazi katika maeneo hayo kuondoka mara moja kutokana na oparesheni ya kijeshi inayotarajiwa kufanyika.
Soma pia:Jeshi la Israel laendeleza mashambulizi Gaza na Lebanon
Kufutia kuongezeka kwa mashambulizi Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati ameandika kupitia mtandao wa X kwamba, mawasiliano ya kidiplomasia yameendelea kati ya Marekani na Ufaransa kwa lengo la kufufua tamko la kusitisha mapigano kwa muda maalum ili kuanza tena kutafuta suluhu za kisiasa.
Ndani ya Gaza Takriban wapalestina 16 wameuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulizi la anga la Israel kwenye Shule ya Rufaida ambayo inawahifadhi watu waliokimbia makazi yao kufuatia mapigano yanayoendelea.
UN: Watu wamekwama Gaza
Kulingana na Umoja wa Mataifa zaidi ya watu laki nne wamekwama kaskazini mwa Gaza chini ya mashambulizi makali ya mabomu, huku hospitali zikiwa na uhaba mkubwa wa dawa na wafanyakazi zikikabiliwa na idadi kubwa ya wagonjwa. Mmoja wa wakaazi wa Gaza alisema hali ni mbaya.
"Kuna mashambulizi makubwa Beit Lahia, magari ya wagonjwa yalikuja na mume wangu na mwanangu wakaenda kuwahamisha majeruhi." Alisema mwanamama huyo huku akilia.
Soma pia:Umoja wa Mataifa waonya kuhusu hali ya Gaza kujirudia nchini Lebanon
Anasimulia kuwa aliporejea baada ya kwenda kutoa msaada kwa majeruhi wengine alimkuta mume wake na kaka yake wakiwa wametapakaa damu, baada ya kupigwa na makombora.
"Nilimkuta mwanangu hana uso. Nilikuwa katika mshtuko na kupiga kelele.. Mume na mwanangu wamekufa." alisema huku akilia kwa uchungu.
Kufuatia kuongezeka kwa mashambulizi ya Israel nchini Lebanon na Gaza Marekani Ilimtaka mshirika wake huyo wa karibu kuepuka hatua ya kijeshi kama za Gaza nchini Lebanon, baada ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kusema inaweza kukabiliwa na "maangamizi" kama eneo la Palestina.