1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashambulia Gaza, Lebanon na Syria

17 Oktoba 2024

Israel imefanya mashambulizi Gaza, Lebanon na Syria huku mshirika wake mkuu Marekani ikishambulia ngome za waasi wa Kihouthi nchini Yemen.

Mashambulizi makali ya Israel katika mji wa kusini mwa Lebanon wa Nabatiyeh
Mashambulizi makali ya Israel katika mji wa kusini mwa Lebanon wa Nabatiyeh: 16.10.2024Picha: Abbas Fakih/AFP

Jeshi la Israel limeshambulia siku ya Alhamisi kwa mabomu mji mmoja wa pwani ya Syria wa Latakia, ambao ni ngome ya Rais Bashar al-Assad, na kuwajeruhi raia wawili. Shirika la uangalizi wa haki za binadamu la Syria, lenye makao yake makuu nchini Uingereza, limesema uvamizi huo wa Israel ulililenga ghala la silaha linalomilikiwa na Hezbollah.

Israel imefanya mamia ya mashambulizi nchini Syria katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na mashambulizi mengi karibu na mpaka wa Lebanon ambayo yanadhamiria kuvuruga njia kuu ya ugavi wa silaha kwa Hezbollah kutoka Iran hadi Lebanon.

Soma pia: Israel yasema 'maslahi ya taifa' kwanza katika kuijibu Iran

Mashambulizi ya Jumatano ya Israel yaliyoyalenga majengo mawili ya manispaa, yaliwaua watu 16 akiwemo meya wa jiji la Nabatiyeh kusini mwa Lebanon.

Kifaru cha Israel karibu na mpaka wa LebanonPicha: Baz Ratner/AP/picture alliance

Hata hivyo, Hezbollah imesema pia kuwa imefanikiwa kuharibu kifaru cha wanajeshi wa Israel waliokuwa wakijaribu kuingia nchini Lebanon. Wakati huo huo, yUkanda wa Gaza pia umeendelea kukabiliwa na mashambulizi ya Israel ambapo watu 11 wameripotiwa kuuawa.

Katika hatua nyingine, mshirika mkuu wa Israel, Marekani imefanya mashambulizi makubwa ya mabomu kwenye vituo vya kuhifadhia silaha katika maeneo yanayodhibitiwa na Wahuthi nchini Yemen.

Wanamgambo waliopo Syria, waasi wa Huthi nchini Yemen, Hezbollah huko Lebanon na Hamas katika Ukanda wa Gaza ni muungano unaojinasibu wa upinzani dhidi ya Israel na unaofadhiliwa na  Iran , ambayo mnamo Oktoba 1 ilifanya shambulio kubwa la makombora 180 dhidi ya Israel ambayo pia imeapa kulipiza kisasi.

Iran yaionya Israel kutoshambulia maeneo yake

Mkuu wa kikosi cha kijeshi cha Walinzi wa Mapinduzi wa Iran Hossein SalamiPicha: Vahid Salemi/AP/dpa/picture alliance

Mkuu wa kikosi cha kijeshi cha Walinzi wa Mapinduzi wa Iran Hossein Salami ameonya kuwa Tehran itaishambulia tena Israel ikiwa watathubutu kushambulia maeneo yao.

"Iwapo mtafanya kosa na kuyashambulia maeneo yetu, iwe katika kanda au Iran, tutawashambulieni tena vibaya mno. Mnaweza kufikiri kwamba mifumo yenu ya ulinzi wa anga itawakinga, lakini hilo si kweli. Msiiamini mifumo hiyo. Hamuwezi kuyaangamiza mataifa ya Kiislamu na mkabaki salama. Hesabu hizo hazina nafasi kwa Waislamu. Kuweni makini, tunaujua udhaifu wenu. Nanyi mnaujua vizuri, " ameonya Salami.

Salami ameyasema hayo leo Alhamisi alipohudhuria mazishi ya afisa mmoja wa kikosi hicho ambaye aliuawa mwezi uliopita katika shambulizi la Israel kusini mwa Beirut  ambalo pia lilimuua kiongozi mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah. Mivutano hii inayoongezeka inazidisha wasiwasi wa kutokea mzozo mpana zaidi wa kikanda huku juhudi mbalimbali za kimataifa zikiendelea kufanyika ili kuepusha janga hilo katika eneo zima la Mashariki ya Kati.

((Vyanzo: AP, DPAE, RTRE, AFP))