1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashambulia kwa ndege za kivita Kusini mwa Gaza

19 Aprili 2022

Jeshi la Israel limeshambulia kile ilichosema ni maeneo ya kutengeneza silaha za Hamas Kusini mwa Gaza baada ya kudai kundi hilo limerusha roketi dhidi ya Israel Jumatatu.

Israel | Zusammenstöße auf dem Tempelberg in Jerusalem
Picha: Ahmad Gharabli/AFP/Getty Images

Wanamgambo wa Kipalestina walifyetua roketi jana kuelekea kusini mwa Israel kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi wakati yakijitokeza mapambano mengine baada ya msururu wa mashambulizi yaliyosababisha umwagikaji damu katika eneo takatifu la msikiti wa al-aqsa mjini Jerusalem.Jeshi la Israel limejibu shambulizi hilo la roketi hii leo.

Israel imesema imelizuia roketi lililorushwa kutoka palestina na hakuna taarifa zilizotolewa mara moja kuhusu waliouliwa au kujeruhiwa au mali iliyoharibiwa na tukio hilo,ingawa Israel imelinyooshea kidole kundi la wanagambo linalotawala ukanda wa Gaza Hamas kwamba ndilo lililohusika.

Ni kwa mara ya kwanza roketi kufyetuliwa kuelekea Israel tangu mkesha wa mwaka mpya. Jana waziri mkuu Naftali Bennett kabla ya roketi kurushwa kuelekea Israel alisema nchi yake imekuwa mlengwa wa kampeini ya uchochezi inayoendeshwa na Kundi la Hamas.

Picha: Fatima Shbair/Getty Images

.

Hii leo alfajiri Israel ilifanya msururu wa mashambulizi ya angani kwa kutumia ndege za kivita katika eneo la kusini mwa ukanda wa Gaza wakilenga maeneo ya kutengeza silaha za kundi la Hamas.

Hayo yameelezwa na jeshi la Israel lakini pia hakuna taarifa kuhusu watu kujeruhiwa.Saa chache kabla ya mashambulio hayo kiongozi wa kundi la wanamgambo wa jihad ambalo linajinadi kwa  kuwa na maroketi  alitowa onyo fupi akilaani vitendo vya uchokozi vya Israel katika mji wa Jerusalem. Ziad al Nakhala ambaye makaazi yake yako nje ya ardhi ya Palestina amesema vitisho vya kutaka kuimarisha hatua za vikwazo katika mpaka baina ya Israel na Misri dhidi ya watu wa Gaza vilivyowekwa baada ya kundi la Hamas kutwaa madaraka miaka 15 iliyopita,haiwezi kuwanyamazisha katika kile kinachotokea Jerusalem pamoja na katika Ukingo wa Magharibi ambako Israel inakaa kwa mabavu.

Hata hivyo hakuna kundi lolote la wapalestina lililodai kuhusika na shambulizi la Roketi iliyoelekezwa Israel.Mwishoni mwa juma Wapalestina walikabiliana na polisi wa Israel ndani na nje ya eneo la msikiti wa Al Aqsa huko Jerusalem ambako kwa miaka chungunzima limekuwa eneo ambalo ni kitovu cha vurugu na vita baina ya Israel na Palestina.

Picha: AHMAD GHARABLI/AFP
Picha: Abir Sultan/epa/dpa/picture alliance

 Eneo hilo ni sehemu ya tatu takatifu kwa waislamu kadhalika ni eneo takatifu kwa Wayahudi ambao wanaliita  mlima wa hekalu kwa sababu msikiti wa al Aqsa uko juu ya mlima ambako hapo kale  ndiko ilikokuwa hekalu kuu ya Wayahudi.

Ikumbukwe mwaka jana ni maandamano na mapambano katika eneo hili ndiyo yaliyochochea vita vikubwa kabisa vya Israel na Gaza vilivyodumu siku 11. Polisi ya Israel imesema ililazimika kujibu mashambulizi ya mawe yaliyokuwa yakirushwa na wapalestina na kwamba wamejitolea kuhakikisha mayahudi,wakristo na waislamu ambao kwa pamoja mwaka huu ibada zao kuu za pasaka na Ramadhani zimekutana wanaweza kusherehekea kwa usalama katika eneo hilo la ardhi takatifu.

Ingawa kwa upande mwingine wapalestina wanahisi polisi wa Israel kuwepo katika eneo hilo ni uchokozi na wanasema walitumia nguvu kubwa dhidi ya wapalestina.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW