1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashambulia maeneo muhimu ya Hamas

Admin.WagnerD9 Julai 2014

Jeshi la Israel limezidhisha mashambulizi dhidi ya ukanda wa Gaza Jumatano, kwa kuyalipua maeneo kadhaa ya Hamas na kuwauwa watu wasiopungua wanane katika siku ya pili ya operesheni ya kuzuwia mashambulizi ya roketi.

Gazastreifen Israelischer Luftangriff 08.07.2014
Picha: Reuters

Mahambulizi hayo yamesabisha mapigano makali zaidi kati ya Israel na kundi la Hamas tangu vita vya siku nane mwezi Novemba mwaka 2012. Wapiganaji wa Hamas walirusha makombora ndani kabisaa ya Israel, huku Israel ikikusanya maelfu ya wanajeshi kwenye mpaka wa Gaza kujiandaa na uwezekano wa mashambulizi ya ardhini ndani ya eneo la Palestina.

Maafisa wa zimamoto wa wakizima moto baada ya shambulizi la ndege za Israel.Picha: AFP/Getty Images

Tangu mashambulizi hayo yalipoanza siku ya Jumanne, Israel imeyashambulia maeneo zaidi ya 400 mjini Gaza, na kuwauwa watu wasiopungua 32. Mashambulizi hayo ya angani na majini, yalianza baada ya wapiganaji wa Hamas kufyetua zaidi ya maroketi 160 ndani ya Israel, likiwemo moja lilikwenda hadi mji wa kaskazini wa Hadera kwa mara ya kwanza. Mji huo uko umbali wa kilomita 100 kutoka Gaza.

'Tuliwaonya Hamas'

Jeshi la Israel limesema kuwa limeshambulia vituo zaidi ya 160 mapema leo, vikiwemo 118 vya kufyetulia maroketi, majengo sita ya Hamas yakiwemo ya polisi ya majini na usalama wa taifa - vituo 10 vya kamandi za kijeshi na ghala za silaha, na njia 10 za chini ya ardhi zinazotumiwa na wapiganaji kwa shughuli za kijeshi na kusafirisha mahitaji kutoka Misri.

"Tulijaribu kupunguza mgogoro huu, tulituma ujumbe kwa Hamas tukawaambia wakomeshe mashambulizi ya roketi lakini wakaendela na sasa tunachukuwa hatua. Viko vya ulinzi vya Israel vinachukuwa hatua ili kuleta hali ambapo watu wa israel hawataishi tena kwa hofu," alisema Mark Regev, msemaji wa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Afisa wa afya mjini Gaza Ashraf Al-Kedra, amesema mashambulizi ya leo yamemuuwa mtu mmoja kusini mwa Gaza, na pia mpiganaji wa kundi la Islamic Jihadi, mama yake na ndugu zake wanne kaskazini mwa Gaza. Mwanaume mwingine aliuwawa akiwa kwenye pikipiki, lakini hakuweza kutambuliwa mara moja.

Maafisa wa polisi wa Israel wakiagalia eneo lilikoanguka roketi mjini Tel Aviv.Picha: Reuters

Jeshi la Israel limesema kuwa ni maroketi manne tu yaliyofyetuliwa kutoka Gaza kwenda Israel usiku wa kuamkia leo, ikiwa ni upungufu mkubwa kutoka idadi kubwa iliyoitikisa miji ya Israel usiku uliyotangulia, na kusababisha vin'gora mjini Jerusalem, Tel Aviv na maeneo mengine.

Jordan yataka kukomeshwa mara moja kwa mashambulizi

Jordan, ambayo ni moja kati ya mataifa mawili tu ya kiarabu yaliyosaini makubaliano ya amani na Israel, imetaka kukomeshwa mara moja kwa mashambulizi dhidi ya Gaza.

Msemaji wa serikali Mohammad Momani amesema mashambuli hayo ambayo yamewauwa Wapalestina zaidi ya 20 katika kile kinachodaiwa kuwa ni kujibu mashambulizi ya roketi ambayo hayamuuwa hata Muisrael mmoja ni ukatili.

Rais wa Marekani Barack Obama pia amezitaka pande mbili kutumia busara na kuacha kulipizana visasi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe,ape
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi