1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashambulia makaazi ya kiongozi wa Hamas

Angela Mdungu
16 Novemba 2023

Jeshi la Israel limesema limeyashambulia makazi ya kiongozi wa kisiasa wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh katika Ukanda wa Gaza. limesema makazi hayo yalikuwa yakitumika kama sehemu ya miundombinu ya kigaidi.

Vifaru vya jeshi la Israel vikiwa Ukanda wa Gaza
Vifaru vya jeshi la Israel vikiwa Ukanda wa GazaPicha: IDF/Handout via Xinhua/picture alliance

Kulingana na jeshi la Israel, makazi hayo ya Haniye mara kwa mara yalitumika kama eneo la mikutano ya viongozi wa juu wa Hamas. Jeshi hilo limesema makazi hayo yalikuwa yakitumika kama sehemu ya miundombinu ya kigaidi na mara kwa mara yalitumika kama eneo la mikutano ya viongozi wa juu wa Hamas.

Jeshi la Israel limebainisha kwamba ndege zake za kivita zimeyashambulia makaazi ya Ismail Haniye anayeongoza Ofisi ya masuala ya kisiasa ya kundi la Hamas. Taarifa za mashambulizi hayo zimetolewa katika chapisho lililoambatana na video ya mashambulizi hayo katika ukurasa wa jeshi la Israel la mtandao wa kijamii wa X uliokuwa ukijulikana awali kama twitter. 

Hata hivyo duru za habari zinasema, Haniyeh,ambaye makazi yake yamelengwa na mashambulizi ya Israel amekuwa akiishi nchini Qatar tangu mwaka 2019 pamoja na familia yake. Kulingana na ripoti kutoka vyanzo ndani ya Hamas, hakukuwa na mtu ndani ya nyumba hiyo wakati wa mashambulizi.

Soma zaidi: Jeshi la Israel ladai kupatikana kwa silaha katika hospitali ya Al-Shifa iliyoko ukanda wa Gaza

Wakati hayo yakijiri, Rais wa Israel Isaac Herzog amezungumzia mustakabali wa hali ya usalama ya Ukanda wa Gaza inavyoweza kuwa hapo baadaye. Herzog amesema Israel haiwezi kuondoka kirahisi Gaza kwani eneo hilo haliwezi kuachwa namna lilivyo sasa. Amefafanaua zaidi na kuongeza kuwa ili kuzuia ugaidi kujitokeza tena, wanapaswa kuwa na kikosi madhubuti kuhakikisha kuwa shambulio kama la Oktoba 7 halijitokezi tena.

Operesheni ya ardhini ya Israel ikiendelea Ukanda wa GazaPicha: Israel Defense Forces/AP Photo/picture alliance

Katika tukio jingine, vikosi vya Israel vimesambaza vipeperushi vinyavyowatahadhrisha Wapalestina kuelekea Kusini mwa Gaza hali inayoashiria kufanyika kwa operesheni kubwa zaidi kuelekea maeneo ambayo maelfu ya watu  waliotii amri ya kuhama wamefurika hasa kwenye hifadhi za Umoja wa Mataifa na nyumba binafsi.

Upekuzi katika hospitali ya Al Shifa unaendelea

Wakati huohuo vikosi hivyo vya Israeli vimeendelea na upekuzi ulioanza tangu Jumatano katika hospitali ya Al-Shifa ingawa hadi sasa haijapata ushahidi wa kuwepo kwa makao makuu ya kamandi ya Hamas  ambayo imesema yako chini ya jengo hilo.

Soma zaidi: Wanajeshi wa Israel waingia katika hospitali kuu ya Gaza

Nalo baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanikiwa kupata muafaka wa azimio kuhusu vita kati ya Israel na Hamas baada ya majaribio kadhaa inayotoa wito wa kusititisha haraka mapigano kwa muda ili kuruhusu misaada ya kiutu iwafikie wakaazi wa Gaza.

Azimio hilo lililopitishwa bila kura ya turufu ya Urusi, Marekani na Uingereza, ilizitaka pande zote za mzozo kuwalinda raia hasa watoto. Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Gilad Erdan alilaani azimio hilo alilolielezea kuwa haliendani na uhalisia.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW