1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashambulia tena Syria

5 Mei 2013

Israel imefanya shambulio la roketi dhidi ya kituo cha utafiti wa sayansi cha Jamraya kilichoko karibu na mji mkuu Damascus usiku wa kuamkia Jumapili,(05.05.2013), limeeleza shirika la habari la Syria SANA.

An Israeli F-15 I fighter jet launches anti-missile flares during an air show at the graduation ceremony of Israeli pilots at the Hatzerim air force base in the Negev desert, near the southern Israeli city of Beersheva, on December 27, 2012. AFP PHOTO / JACK GUEZ (Photo credit should read JACK GUEZ/AFP/Getty Images)
Ndege za kivita za Israel zikishambulia ndani ya SyriaPicha: Getty Images

Shirika hilo halikusema iwapo kuna watu ambao wameuwawa ama kujeruhiwa. Shambulio hilo la Israel lililenga katika kulegeza hali ya kuzingirwa kwa magaidi katika upande wa mashariki ya jimbo la Ghouta, karibu na Damascus, imeongeza televisheni ya Syria.

Iwapo itathibitishwa, shambulio hilo litakuwa la pili la Israel kwa wiki hii dhidi ya Syria. Ripoti za vyombo vya habari vya Marekani zinasema kuwa Israel ililenga shehena ya silaha iliyokusudiwa kupelekwa kwa wanamgambo wa Hizboullah katika nchi jirani ya Lebanon usiku wa Alhamis kuamkia Ijumaa, lakini taifa hilo la Kiyahudi limekataa kuthibitisha ama kukana shambulio hilo la mabomu.

Makombora yaharibiwa

Duru za kidiplomasia nchini Lebanon zimeliarifu shirika la habari la AFP kuwa operesheni hiyo iliharibu makombora yanayorushwa kutoka ardhi hadi angani yaliyopelekwa nchini Syria na Urusi ambayo yalikuwa yamehifadhiwa katika uwanja wa ndege wa Damascus.

Rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: Reuters

Israel imethibitisha kuwa imefanya shambulio hilo la anga dhidi ya Syria mwishoni mwa mwezi wa Januari wakati rais Bashar al-Assad alipoishutumu Israel kwa kujaribu kuidhoofisha zaidi nchi yake iliyoharibiwa kwa vita.

Shambulio hilo la anga lilishambulia makombora hayo pamoja na eneo la kijeshi la karibu na hapo ambalo linaaminika kuwa linahifadhi silaha za kemikali, kama maafisa wa Marekani walivyosema wakati huo.

Syria yatishia

Syria imetishia kulipiza kisasi , hali inayozidisha zaidi hofu ya vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe kusambaa katika eneo hilo, ambapo Umoja wa Mataifa umesema umesababisha watu 70,000 wameuwawa tangu Machi mwaka 2011.

Wanaharakati , wakati huo huo , wamesema kuwa miili ya raia 62, ikiwa ni pamoja na watoto, iligunduliwa katika bandari ya kaskazini magharibi ya Banias siku moja baada ya shambulio lililofanywa na majeshi ya serikali na muungano wa kitaifa wa upinzani umeonya dhidi ya kile ilichokiita , "mauaji ya maangamizi."

Marekani haiamini kuwa ndege za kivita za Israel zimeingia katika anga ya Syria wakati wa shambulio hilo, kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha CNN, Marekani na mashirika ya kijasusi ya mataifa ya magharibi.

Israel ina haki ya kujilinda

Rais wa Marekani Barack Obama , akizungumza na kituo cha televisheni cha lugha ya Kihispania , amesema kuwa Israel ina haki katika kujilinda dhidi ya usafirishaji wa silaha kwenda kwa kundi la Hizboullah.

Jeshi la Lebanon limesema kuwa ndege mbili za kijeshi za Israel ziliingia katika anga lake mara tatu siku ya Alhamis usiku na kubaki humo kwa muda wa saa mbili ama tatu.

Shirika la habari la Syria SANA, likielezea kuhusu taarifa za awali , limesema mapema leo Jumapili kuwa makombora ya Israel yameshambulia kituo cha utafiti wa kijeshi karibu na mji mkuu Damascus.

Iwapo itathibitishwa , litakuwa shambulio la pili nchini Syria katika muda wa siku tatu, ikiashiria kuongezeka kwa uhusika wa Israel katika mzozo wa Syria.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / afpe

Mhariri: Sudi Mnette

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi