1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yashutumiwa kwa unyanyasaji wa wafungwa

Hawa Bihoga
13 Agosti 2024

Umoja wa Mataifa, mashirika ya kutetea haki za binaadamu ndani ya Palestina na Israel na vyombo vya habari vimekuwa vikitoa tahadhari ya madai kuhusu unyanyasaji, mateso kwa Wapalestina wanaozuiliwa magereza ya Israel.

Israel -Hebron
Wanajeshi wa Israel huko Ukingo wa MagharibiPicha: Wisam Hashlamoun/picture alliance

Kiini cha madai hayo ni kituo cha kimoja cha kijeshi kusini mwa Israel ambacho kilianzishwa kushughulikia washukiwa wanaounga mkono wanamgambo baada ya shambulizi la Hamas na kundi washirika la Islamic Jihad dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023, ambalo lilisababisha takribani watu 1,140 kuuawa na zaidi ya 240 kuchukuliwa mateka.

Wiki mbili zilizopita, wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Israel wakiwemo wabunge, walivamia vituo viwili vya kijeshi, ambavyo ni Sde Teiman na Beit Lid na mahakama ya kijeshi, kusini mwa taifa hilo, wakionesha mshikamano kile kilichotajwa kushikiliwa kwa wanajeshi tisa wa jeshi la Israel ambao wanahojiwa na jeshi kwa tuhuma za kumbaka na kumfanyia dhuluma zingine mwanamume mmoja wa Kipalestia anayeshikiliwa katika kituo cha Sde Teiman.

Soma: Israel yashutumiwa kwa mauaji ya halaiki baada ya shambulizi la shule moja mjini Gaza

Kituo cha habari cha Channel 12 cha Israel kilichapisha video hivi karibuni inayoonesha dhuluma dhidi ya mfungwa huyo. Hata hivyo, mjadala mpana uliozuka kufuatia kuvamiwa kwa kituo hicho unaonesha ni kwa namna gani ushawishi wa siasa za mrengo wa kulia unavyozidi kukuwa, huku Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akitoa wito wa utulivu, katika wakati ambao baadhi ya wanasiasa wakitaka wanajeshi hao wanaotuhumiwa kupewa kinga.

Vifaru vya Israel Ukanda wa GazaPicha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Kisa hicho kimefichua kwa mara nyingine unyanyasaji kwa Wapalestina katika vizuizi na magereza ya Israel, madai ambayo yamezidi kuongezeka katika miezi ya hivi karibuni. Ushuhuda wa kwanza wa unyanyasaji katika kituo cha Sde Teiman ulifichuliwa mnamo Desemba mwaka uliopita, baada ya madaktari wa Israel ambao walikuwa wakitoa huduma katika kituo hicho kusema kwamba wafungwa wengi hawakuelezwa wapi hasa walipo.

Profesa Yoel Donchin ambae ni miongoni mwa madaktari anayehudumu katika kituo cha Sde Teiman anasema watu wengi waliuawa kwa sababu tu walishukiwa.

"Wakamateni na muwauwe, ama wakamateni na kuwapeleka mahakamani, lakini kuwapeleka hospitali ama kuwadhulumu? Kwa sababu wao ni Waarabu? Huwezi kujua nani anaekuja huwezi kujua iwapo walikuwa wakiwaleta mateka... kuanza kuwahoji hawawezi kuzungumza... watu wetu waliuawa kwa sababu walishukiwa, mimi si sehemu ya kufanya unyama."

Kwa upande mwingine shirika la madaktari wanaotetea haki za kibinaadamu nchini  Israel, limechapisha ripoti kadhaa kuhusu madai ya unyanyasaji katika miezi iliyopita. Mkurugenzi wa shirika hilo, Naji Abbas, amesema kwamba macho ya wafungwa hao yalifungwa wakati wote kwa miezi kadhaa kwa masaa 24 huku mikono yao ikiwa imefungwa nyuma muda wote na kuongeza kwamba hakuna mtu ambae alikuwa anafahamu kuhusu eneo hilo. Israel yafanya operesheni mpya ya kijeshi Khan Younis

Aidha shirika hilo liliiambia DW kwamba limepata nakala ya miongozo iliyotolewa na Wizara ya Afya ya Israel ambayo ilisema wafungwa wanapaswa kusalia  wamefungwa pingu wakati wa matibabu na madaktari hawapaswi kusajili majina yao kwenye orodha ya matibabu.

Umoja wa Mataifa wasema Israel haizingatii ulinzi wa raia. Nayo Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema wafungwa walizuiliwa katika "vizuizi na kuvuliwa nguo." Ripoti hiyo iliongeza kwamba kumekuwa na visa vya kunyimwa chakula, kuzuiwa kulala usingizi, kumwagiwa maji na kupigwa shoti ya umeme kadhalika kuchomwa na sigara. Baadhi ya wafungwa walisema mbwa waliachiliwa kuwadhuru.

Shambulizi la roketi lauwa watu 12 katika milima ya Golan

01:03

This browser does not support the video element.

Katika ripoti yenye jina "Karibu Kuzimu," shirika la kutetea haki za binadamu la Israel, B'Tselem, lilisema unyanyasaji umekuwa wa kawaida katika magereza mengi nchini humo. Shirika hilo lilisema limekusanya shuhuda kutoka kwa Wapalestina 55 waliokuwa wakishikiliwa katika magereza ya Israel na baadaye kuachiliwa, bila kufunguliwa mashtaka.

Soma: Jeshi la Israel laamuru watu kuondoka kusini mwa Gaza

Hata hivyo jeshi la Magereza Israel limekanusha madai hayo na kuisisitizia DW kwamba "linafanya kazi kwa mujibu wa masharti ya sheria na chini ya usimamizi wa mdhibiti wa serikali." Kuhusiana na wanajeshi wa Israel kumbaka mwanamume wa Kipalestina, jeshi lilisema kwamba wameomba kuongeza muda wa kuzuiliwa kwa wanajeshi watano wanaoshukiwa kwa unyanyasaji huo wa kingono ili kufanikisha uchunguzi wa mkasa huo.

Vyombo vya habari Israel vimeripoti mfungwa huyo tayari ametolewa hospitali na kurejeshwa tena katika kizuizi cha kijeshi cha Sde Teiman.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW