1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yataka Iran isilegezewe masharti kuhusu nyuklia

29 Novemba 2021

Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennet amezitolea mwito nchi zenye nguvu zaidi duniani zisilegeze kamba kuhusu hujuma ya Iran mnamo wakati mazungumzo ya kufufua mkataba wa nyuklia wa Iran yameanza mjini Vienna.

Israel Naftali Bennett Premierminister
Picha: Gil Cohen-Magen/AP/picture alliance

Wawakilishi wa nchi zilizosalia kwenye makubaliano hayo, ambazo ni Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Urusi na China watakutana katika hotel ya kifahari ya Palais Coburg ambapo makubaliano hayo yalisainiwa miaka sita iliyopita.

Wajumbe wa Marekani wanaoongozwa na Robert Malley wanashiriki mazungumzo hayo japo si kwa njia ya moja kwa moja.

Akiwasilisha wito wake kwa njia ya video kwa wawakilishi wa mazungumzo hayo, Naftali Bennett amesema Tehran inataka vikwazo dhidi yake viondolewe lakini bila kuridhia masharti dhidi yake.

   "Licha ya Iran kukiuka makubaliano ya nyuklia na pia inavyohujumu shughuli za ukaguzi, Iran itkuwepo katika meza ya majadiliano mjini Vienna, na wapo wale wanaofikiri kuwa vikwazo dhidi ya Iran vinafaa kuondolewa na kisha mabilioni ya dola yamiminike kwenye utawala huo mbovu,” amesema Bennett.

Iran imeendelea kuzidisha urutubishaji wa madini ya urani tangu Marekani ilipojiondoa kwenye mkataba huo mwaka 2018.Picha: picture-alliance/dpa/EPA/STR

Hayo yanajiri wakati washauri wa mazungumzo hayo wakikutana mjini Vienna Austria kuanza duru nyingine ya majadiliano yanayolenga kufufua makubaliano ya kimataifa ya mwaka 2015 kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Israel yapinga mkataba wa nyuklia na Iran

Israel imejitokeza kimasomaso kuupinga mkataba huo na maafisa wake wanasema Iran inakaribia zaidi sana kutengeneza zana za kinyuklia kuliko wakati wowote ule. Hatua inayosema haitakubaliana nayo

Waziri wa mambo ya nje wa Israel Yair Lapid anayeizuru Uingereza wiki hii kujadili suala la Iran akiwa na maafisa wa usalama wa Uingereza na Ufaransa.

Waziri wa Ulinzi wa Israel Benny Gantz pia ataelekea Washington wiki hii kujadili suala hilo hilo.

Iran inasisitiza kwamba mpango wake wa nyuklia ni wa amani pekee. Inaulaumu uamuzi wa uliokuwa utawala wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump wa kujitoa na kurudisha vikwazo kwa Iran kwamba ndio ulisababisha mkataba huo kuvunjika.

Rais wa Marekani Joe Biden ameashiria kutaka kuirudisha nchi yake kwenye makubaliano hayo.Picha: Michael Reynolds/Pool via CNP/picture alliance

Israel inatizamwa pakubwa kuwa nchi pekee inayomiliki zana za kinyuklia katika Mashariki ya Kati, japo inashikilia será isiyoeleweka bayana kuhusu mpango wake wa ikiwa inamiliki au la.

Matumaini ya matokeo chanya kwenye mazungumzo hayo ni finyu

Duru ya mwisho ya mazungumzo hayo yanayolenga kuiwezesha Iran kuheshimu masharti yaliyowekwa dhidi yake na pia kuirudisha Marekani kwenye mkataba huo ilifanyika mwezi Juni. Tangu wakati huo, juhudi hizo zimeendelea kukumbwa na changamoto.

Makubaliano hayo yaliifanya Iran kuacha kurutubisha madini ya urani baada ya vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi yake kuondolewa. Lakini tangu makubaliano yalipoporomoka, Iran imeendelea kurutubisha madini hadi kwa kiwango cha asilimia 60, ambayo inakaribia kiwango kinachoweza kutengeneza zana za kivita.

(APE, AFPE)