Israel yataka kufungwa shirika la wakimbizi Palestina
8 Januari 2018Israel pia imeyataja makundi 20 ya wanaharakati duniani kote ambao wanachama wake watapigwa marufuku kuingia nchini humo kuhusiana na miito yao ya kulisusia taifa la Kiyahudi.
Israel kwa muda mrefu inaliona shirika hilo la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina, lijulikanalo kama UNRWA kuwa lina upendeleo dhidi ya nchi hiyo, madai yanayokanushwa vikali na shirika hili, likisema linatoa tu huduma muhimu kwa Wapalestina, UNRWA ni shirika linaloendeleza matatizo ya wakimbizi wa Wapalestina, amesema Netanyahu wakati huohuo akimsifu rais Trump mwanzoni mwa kikao cha baraza la mawaziri cha kila wiki.
Amesema wakati mamilioni ya wakimbizi wengine duniani kote wanapatiwa huduma na shirika la Umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR , Wapalestina wana shirika lao ambalo pia linawahudumia "wajukuu wa wakimbizi ambao kwa mtazamo wake si wakimbizi.
Hali hii isiyoeleweka ni lazima ifikie mwisho," Netanyahu alisema.
Kauli ya Netanyahu yapingwa
"Pendekezo langu liko wazi , kuipatia fedha UNRWA ni lazima kuhamishiwe taratibu katika shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR , kwa utaratibu maalum wa kusaidia wakimbizi wa kweli na sio wale ambao si wa kweli, kama inavyotokea leo chini ya UNRWA."
Msemaji wa UNRWA Chris Gunness amesema kwamba mamlaka ya shirika hilo yametolewa na baraza kuu la Umoja wa Mataifa, ambalo wanachama wake wanatoa uungaji mkono mkubwa kwa shirika hilo la kutoa misaada ya maendeleo na kiutu".
"Kile kinachoendeleza mzozo wa wakimbizi ni kushindwa kwa pande hizo kushughulikia suala lenyewe," aliandika katika taarifa.
"Hali hii inapaswa kutatuliwa na pande zinazohusika na mzozo huo katika muktadha wa mazungumzo ya amani, yaliyo chini ya maazimio ya Umoja wa mataifa na sheria za kimataifa," amesema Chris Gunness.
Mwezi Juni , Netanyahu alisema alilizungumza suala hilo pamoja na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley.
Wanaharakati kupigwa marufuku
Wakati huo huo Israel mwaka jana ilipitisha sheria ambayo itapiga marufuku mwanaharakati yeyote ambaye "kwa makusudi kabisa anatoa wito wa kuisusia Israel." Orodha iliyotolewa jana Jumapili, ambayo inajumuisha shirika lililotuzwa nishani ya amani ya Nobel , inaambatana na sheria hiyo.
"Mashirika yanayotaka Israel itengwe yanapaswa kutambua kwamba taifa la Israel litachukua hatua dhidi yao," amesema waziri wa mikakati Gilad Erdan katika taarifa. Orodha ya makundi hayo ni kutoka Marekani, Ufaransa, Afrika kusini na kwingineko.
Kamati ya Marafiki wa Marekani wa kutoa huduma , kundi ambalo limo katika orodha hiyo , limesema litaendelea kufanyakazi kwa ajili ya "amani na haki." Kundi hilo pamoja na shirika la Quaker la Uingereza yalishinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1947 kwa kuwasaidia wakimbizi wa vita vikuu vya dunia.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / afpe
Mhariri: