Israel yataka nguvu za kijeshi kutumika dhidi ya Iran
23 Septemba 2022Kwenye jukwaa la Baraza Kuu ya Umoja wa Mataifa, Yair Lapid aliushutumu uongozi wa Tehran kwa kuendesha kile alichodai kuwa ni "harakati za chuki dhidi ya Wayahudi." Lapid amesema wanaitikadi wa Iran wanawachukia na kuwaua Waislamu wenye mawazo tofauti, akitaja mfano wa Salman Rushdie na Mahsa Amini, mwanamke ambaye kifo chake baada ya kukamatwa na maafisa wa polisi ya maadili ya Iran kimesababisha maandamano makubwa nchini humo.
''Dunia haito jibu kwa maneno lakini kwa nguvui za kijeshi''
Waziri Mkuu wa Israel amesema njia pekee ya kuizuia Iran kupata silaha za nyuklia ni kuweka vitisho vya kuaminika vya kijeshi.
''Endapo utawala wa Iran utapata silaha za nyuklia watazitumia. Njia pekee ya kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia ni kuweka kitisho cha kuaminika cha kijeshi mezani. Na kisha tu, kujadiliana nao mapatano marefu na yenye nguvu zaidi. Inabidi ifahamike wazi kwa Iran kwamba iwapo itaendeleza mpango wake wa nyuklia, dunia haitojibu kwa maneno lakini kwa nguvu za kijeshi." alisema Lapid.
Israel, ambayo inaichukulia Iran kuwa adui wake mkuu, pia inailaumu Tehran kwa kufadhili mavuguvugu wanayoyaita "makundi ya watu wenye silaha", zikiwemo Hezbollah ya Lebanon na Hamas ya Palestina. Israel katika siku za karibuni imekuwa ikifanya juhudi za kidiplomasia za kujaribu kuishawishi Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuachana na mpango wa kuufufua mkataba wa nyuklia wa Iran wa mwaka 2015.
Mataifa mawili
Kuhusu mzozo baina ya Isarel na Palestina, Yair Lapid amesema licha ya vikwazo vilivyopo, makubaliano na Wapalestina, yenye msingi wa mataifa mawili kwa watu wa Israel na Palestina, ni jambo sahihi kwa usalama wa Israel, kwa uchumi wa Israel na kwa mustakabali wa watoto wa nchi hiyo.
Lapid, ambaye anafanya kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa bunge wa Novemba 1, alisema idadi kubwa ya Waisraeli wanaunga mkono suluhisho la serikali mbili ikiwa ni pamoja na yeye binafsi. Israel kwenyewe, hotuba ya Waziri Mkuu ilikosolewa na wapinzani wake wa kisiasa.
Rais wa Marekani Joe Biden, hata hivyo, aliikaribisha hotuba hiyo ya Lapid na kuiita kuwa ni uungwaji mkono wa ujasiri kwa suluhisho la mataifa mawili. Jumatano, Biden aliunga mkono juhudi mpya za kuanzishwa kwa taifa la Palestina lakini hakutoa dalili yoyote ya mpango mpya wa amani. Mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina yamekwama tangu mwaka 2014.