1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yathibitisha kumuua Yahya Sinwar

17 Oktoba 2024

Israel imethibitisha jioni ya Alhamisi (17.10.2024) kuwa imemuua kiongozi mpya wa kundi la Hamas Yahya Sinwar kufuatia operesheni yao katika Ukanda wa Gaza.

Kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar
Kiongozi wa Hamas Yahya SinwarPicha: Mohammed Talatene/dpa/picture alliance

Serikali ya Israel kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje Israel Katz imethibitisha kumuua Yahya Sinwar. Awali, jeshi la Israel lilikuwa likisubiri vipimo vya vijinasaba (DNA) ili kuthibitisha utambulisho kiongozi huyo aliyeuawa.

Sinwar, anachukuliwa kama mratibu mkuu wa shambulio la Oktoba 7 mwaka 2023 dhidi ya Israel ambalo lilisababisha vifo vya karibu watu 1,200 huku mamia ya wengine wakichukuliwa mateka. Alichukua nafasi hiyo kufuatia mauaji ya mtangulizi wake Ismail Haniyeh aliyeuawa mjini Tehran mwezi Agosti.

Kauli za viongozi mbalimbali duniani 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema: "Sinwar alikuwa muuaji katili na gaidi, ambaye alitaka kuiangamiza Israel na watu wake. Kauli kama hizo zimetolewa pia na viongozi wa Marekani na Uingereza waliotaja kuwa Sinwar alisababisha mateso kwa Wapalestina na Waisraeli.

Waziri wa mahusiano ya kigeni wa Italia Antonio Tajani amesema: “Natumai kutoweka kwa kiongozi wa Hamas kutazidisha uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza."

Israel yaendeleza mashambulizi huko Gaza

Watu 14 wameuawa hii leo kaskazini mwa Ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel kwenye shule ya Abu Hussein huko Jabalia, ambayo inatumiwa kuwahifadhi Wapalestina walioyakimbia makazi yao. Miili ilipelekwa katika hospitali za Kamal Adwan na ile ya Al-Awda, huku Israel ikidai kuwa ilikuwa ikiwalenga wanamgambo wa Hamas na wale wa Islamic Jihad.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas imesema kufikia sasa mzozo huo umesababisha vifo vya watu 42,438, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.  Umoja wa Mataifa umekuwa ukisema kwamba idadi hiyo ni ya kuaminika, na leo hii umetahadharisha pia kuwa takriban raia 345,000 wa Gaza wanakabiliwa janga la njaa hasa msimu huu wa baridi kutokana na kupungua kwa utoaji wa misaada.

Ujerumani kuendelea kuipatia Israel silaha 

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akisalimiana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Michael Sohn/AP/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema nchi hiyo itaendelea kuisaidia Israel kujilinda kwa kuipatia silaha, lakini akasema ni lazima ifuate sheria za kimataifa na kuzingatia lengo kuu la kuwepo suluhisho la mataifa mawili. Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Ujerumani imeidhinisha mauzo ya silaha kwa Israel yenye thamani ya karibu dola milioni 34.

Soma pia: ICJ yakataa ombi la kuizuwia Ujerumani kuipa silaha Israel

Tukielekea kidogo huko Lebanon, serikali mjini Tel-Aviv imeeleza kuwa katika muda wa saa 24 zilizopita, wanamgambo 45 wa Hezbollah wameuawa. Lakini Israel imekuwa ikikabiliwa na ukosoaji mkubwa kufuatia hatua zake huko Mashariki ya Kati. Mkuu wa sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amesema umoja huo unapaswa kuchukua hatua madhubuti katika kuushughulikia mzozo wa Mashariki ya Kati, huku Waziri Mkuu wa Ireland Simon Harris, akisema kuwa maneno matupu hayatoshi.

"Na ulimwengu hauchukui hatua za kutosha kuweka mazingira ya kuwezesha usitishwaji mapigano. Na tumekuwa mara kwa mara tukihudhuria mikutano kama hii, ambayo kimsingi ina nia njema, na kauli nyingi zimekuwa zikitolewa. Lakini hatua ambazo zingeliweza kuchukuliwa, hazikuchuliwa, " amesisitiza Harris.

Kwa upande wake, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Jordan, Marwan Muasher ambaye sasa ni Naibu kiongozi wa taasisi ya Carnegie inayofuatilia masuala ya amani kimataifa, ameiambia DW kuwa kwa sasa diplomasia imeshindwa huko  Mashariki ya Kati  na njia pekee ya kuumaliza mzozo huu ni kukomesha vitendo vya ukaliaji kimabavu katika maeneo ya Palestina.

(Vyanzo: Mashirika)

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW