1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yatishia kushambulia Rafah wakati wa Ramadhan

19 Februari 2024

Israel imetishia kuvamia mji wa Rafah ndani ya Ukanda wa Gaza ifikapo mwanzo wa mwezi mtukufu kwa Waislamu wa mfungo wa Ramadhan, endapo mateka wanaoshikwa na wanamgambo wa Hamas hawatakuwa wameachiliwa huru.

Benny Gantz, waziri katika baraza la Mawaziri wa Vita la Israel
Benny Gantz, waziri katika baraza la Mawaziri wa Vita la IsraelPicha: Debbie Hill/ UPI Photo/Newscom/picture alliance

Kwingineko Mahakama ya Haki ya Umoja wa Mataifa imeanza kuskiliza kesi ya kihistoria dhidi ya Israel kuhusu uhalali wake kuikalia ardhi ya Palestina kimabavu. 

Huku matarajio ya mazungumzo ya mapatano yakiwa yamefifia, Marekani, serikali nyinginezo, pamoja na Umoja wa Mataifa, zimetoa wito wa dharura kwa Israel kusitisha mashambulizi yake yaliyopangwa dhidi ya Rafah.

Soma: Israel yakabiliwa na shinikizo jipya kutoka Marekani dhidi ya kuishambulia Rafah

Kulingana na serikali ya Israel, mji wa Rafah ulioko katika mpaka wa Gaza na Misri, ndio ngome ya mwisho iliyosalia ya wanamgambo wa Hamas.

Onyo la Israel limejiri licha ya shinikizo la kimataifa kutaka raia wengi wa Gaza waliokimbilia mji huo wa kusini mwa Gaza Rafah, walindwe.

Wahamiaji wengi wa Gaza walikimbilia mji wa Rafah

Inakadiriwa kuwa robo tatu ya watu wote waliohamishwa na vita Gaza, walikimbilia Rafah, wakiishi kwenye mahema bila huduma za msingi za kutosha ikiwemo chakula, dawa na maji.

Soma pia: Wasiwasi wa kimataifa waongezeka kufuatia operesheni ya Israel Rafah

Hospitali katika Ukanda wa Gaza zaelemewa

02:03

This browser does not support the video element.

Benny Ganz, waziri katika baraza la Mawaziri wa Vita la Israel amesema wanamgambo wa Hamas wanaweza kuchagua kati ya kujisalimisha au kuwaachilia huru mateka ili raia wa Gaza wafunge Ramadhan kwa amani.

"Ikiwa wanaoshikiliwa mateka hawatakuwa wameachiliwa huru ifikapo Ramadhani, mapigano yataendelea kotekote ikiwemo eneo la Rafah. Tutafanya hivyo taratibu, kuwezesha kuhamishwa kwa raia kuondoka, kwa mazungumzo na washirika wetu wakiwemo Marekani na Misri na kupunguza vifo vya raia kadri iwezekanavyo," amesema Ganz.

Vita vya Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas vilianza baada ya kundi hilo kufanya shambulizi baya kusini mwa israek mnamo oktoba 7.

Soma pia: Mahakama ya UN yaitaka Israel kuepusha mauaji ya kimbari Gaza

Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya miongoni mwa mataifa mengine yameliorodhesha hamas kuwa kundi la kigaidi.

Mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Machi.

ICJ yasikiliza kesi dhidi ya Israel kuhusu uhalali wake kukalia ardhi inayodaiwa na Wapalestina.Picha: REMKO DE WAAL/ANP/AFP

ICJ yasikiliza kesi ya dhidi ya Israel ya kukalia ardhi inayodaiwa na Wapalestina

Katika tukio jingine, mahakama ya Haki ya Umoja wa Mataifa imeanza kusikiliza kesi ya kihistoria Jumatatu dhidi ya Israel, kuhusu uhalali wake wa kukalia kimabavu kwa miaka 57, ardhi inayodaiwa na Wapalestina.

Vikao hivyo vinafuatia ombi lililowasilishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa maoni ya ushauri yasiyofungamana na sera za Israeli katika maeneo yaliyochukuliwa.

Mawakili wa upande wa mamlaka ya Wapalestina wanatarajiwa kuiambia mahakama hiyo ya kimataifa kwamba Israel imekiuka sheria kwa kunyakua sehemu kubwa ya ardhi yao, kwamba Israel imezuia haki ya Wapalestina kuwa taifa na kuwa imeweka mfumo wa ubaguzi na utawala wa rangi.

Soma pia: Afrika Kusini yawasilisha hoja zake ICJ dhidi ya Israel

Katika tukio jingine, hsiku ya Jumanne Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litatarajiwa kupiga kura kuhusu rasimu ya makubaliano inayoungwa mkono na nchi za Kiarabu, ya kutaka usitishaji vita mara moja huko Gaza, ili kuwezesha shughuli na huduma za kiutu.

Hata hivyo, tayari Marekani imesema itatumia kura yake ya turufu kuzuia rasimu hiyo.

Vyanzo: APE, AFPE, AFPTV

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW