1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yatoa onyo kali kwa Iran, Tehran yasema ni porojo tu!

8 Mei 2025

Israel imeionya Iran kuwa itafanya kile ilichofanya kwa kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza, baada ya shambulizi katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion lililofanywa na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran.

Milima ya Golan | Netanyahu na Katz
Israel inashtumu iran kuwawezsha Wahouthi kufanya shambulio ambalo lilishindwa kuzuwiwa na mifumo yake ya ulinzi wa anga.Picha: Kobi Gideon/Israel Gpo via ZUMA Press Wire/picture alliance

Israel imeionya Iran kuwa inaweza kuikabili vikali kwa njia ile ile ilivyolishughulikia kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza, kufuatia shambulizi lililofanyika kwenye uwanja wa ndege wa Ben Gurion na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Tehran.

Hili linakuja huku kukiwa na hatua nyingine za Israel dhidi ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, likiwemo kufungwa kwa shule zake tatu katika Jerusalem Mashariki.

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema Iran inawajibika moja kwa moja kwa shambulizi la karibuni katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion, akisema ni wazi kuwa Iran ndiyo inayowafadhili Wahouthi kwa silaha na fedha.

Katika taarifa yake, alisema: "Kilichofanywa kwa Hezbollah huko Beirut, kwa Hamas huko Gaza, na kwa Assad huko Damascus, tunaweza kukifanya Tehran.”

Katz alisisitiza kuwa Israel haiwezi kuvumilia mashambulizi yoyote kutoka kwa wapinzani wake, na ikaweka wazi kuwa itachukua hatua kali dhidi ya tishio lolote kwa usalama wake wa kitaifa.

Kombora lililorushwa na waasi wa Kihouthi wa Yemen liligonga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ben Gurion nchini Israel siku ya Jumapili, na kujeruhi watu wawili pamoja na kusababisha uharibifu.Picha: Chen Junqing/Xinhua/picture alliance

Soma pia: Bahari ya Shamu: Je, meli za kivita za EU zitawazuwia waasi wa Houthi?

Katika kujibu shutuma hizo, serikali ya Iran imekanusha vikali kuhusika na shambulizi la waasi wa Kihouthi dhidi ya uwanja wa ndege wa Ben Gurion karibu na Tel Aviv. Tehran imeeleza kuwa hatua hiyo ni propaganda ya kisiasa inayolenga kuchochea vita vya moja kwa moja kati ya mataifa hayo mawili.

Vikosi vya Israel vyafunga shule za UNRWA Jerusalem Mashariki

Wakati hali ikiwa tete kwa upande wa kijeshi, Israel imechukua hatua za ndani kwa kufunga shule tatu zinazoendeshwa na UNRWA katika Jerusalem Mashariki. Hatua hii inakuja miezi michache baada ya tangazo la kupiga marufuku shughuli zote za shirika hilo ndani ya eneo hilo kuanza kutekelezwa rasmi.

Katika tangazo la serikali, kuanzia Mei 8, 2025, UNRWA imepigwa marufuku kuendesha taasisi zozote za elimu, kuwaajiri walimu, au kuendesha shughuli yoyote ya shule. Aidha, wanafunzi wamezuiwa kuingia shuleni, jambo lililozua taharuki miongoni mwa jamii ya Kipalestina.

Soma pia: Waasi wa Kihouthi wajizolea umaarufu

Fahed Qatousa, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Wavulana ya Shuafat, amesema kufungwa kwa shule wakati mwaka wa masomo unatarajiwa kuisha Juni 20, kunaacha pengo kubwa katika elimu ya watoto.

"Tuna matumaini kwamba uamuzi wa kuzifunga shule utaondolewa kwa sababu huu ni uamuzi usio wa haki kwetu, kwa wanafunzi na wazazi wao, walimu, na kila mtu anayefanya kazi katika shule hii," alisema Qatousa.

Ayatollah ataka Wahouthi kuungwa mkono

00:56

This browser does not support the video element.

Mkurugenzi wa UNRWA katika Ukingo wa Magharibi, Roland Friedrich, amesema vikosi vya Israel vilivyojihami kwa silaha viliizingira shule ya Shuafat mapema leo, na kuzuia ufanyaji kazi wa kawaida wa shule hiyo. Hili ni pigo jingine kwa mfumo wa elimu kwa wakimbizi wa Kipalestina.

Msalaba Mwekundu: Uzuwiaji wa misaada Gaza haukubailiki

Katika hatua nyingine, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imekemea vikali hatua ya Israel kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza. Mkurugenzi Mkuu wa ICRC, Pierre Krahenbuhl, amesema hali hiyo inakiuka sheria ya kimataifa ya haki za kibinadamu.

Akizungumza mjini Geneva, Krahenbuhl alisema: "Ni jambo lisilokubalika kabisa kwamba msaada wa kiutu unazuiliwa wakati watu wanahitaji msaada wa haraka zaidi. Hii ni kinyume na misingi ya ubinadamu.”

Maendeleo haya mapya yanazidisha mvutano katika eneo la Mashariki ya Kati, huku Israel ikiendelea na sera zake za kiusalama dhidi ya vikundi vinavyoungwa mkono na Iran, na mashirika ya kimataifa yakishutumu kukandamizwa kwa huduma za kijamii kwa raia wa Palestina.

Je, hali hii itasababisha mzozo mpya wa wazi kati ya Israel na Iran, au kuna fursa ya kidiplomasia mbele? Dunia inatazama kwa wasiwasi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW