1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel yatofautiana na Marekani kuhusu hatma ya vita Gaza

19 Januari 2024

Israel imetofautiana na mshirika wake mkuu Marekani juu ya uwezekano wa kuundwa taifa huru la Palestina. Washington inasema uwepo wa suluhisho la mataifa mawili ndio njia pekee ya kupatikana amani ya kudumu.

Israel | Antony Blinken akisalimiana na Netanyahu mjini Tel Aviv
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken (kushoto) akiwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Tel Aviv: 09.01.2024Picha: Kobi Gideon/GPO/Anadolu/picture alliance

Israel imepishana kauli waziwazi na mshirika wake mkuu Marekani baada ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kusema nchi hiyo haiko tayari kuona taifa huru la Palestina linaundwa.

Netanyahu ametoa kauli hiyo siku moja tu baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kusema kuwa Israel haitakuwa na "usalama kamili" bila kuandaa njia ya kuelekea  uhuru wa Palestina.

Alipoulizwa na mwandishi wa habari kuhusu msimamo wa Netanyahu wa kupinga kuanzishwa kwa taifa la Palestina baada ya vita hivyo, Msemaji wa Baraza la Usalama la Marekani John Kirby amesema:

Msemaji wa Baraza la Usalama la Marekani John Kirby akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House mjini Washington: 04.01.2024Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

" Ningependa kukueleza tu kwamba hakuna kilichobadilika katika azma ya rais Joe Biden kuhusu suluhisho la serikali mbili ambalo kwa kweli ni kwa manufaa  sio tu ya watu wa Israel lakini pia watu wa Palestina, na hata kwa manufaa ya ukanda ule. Na hatutaacha kufanya kazi kwa lengo hilo. Hii si kauli mapya ya Waziri Mkuu Netanyahu. Ni wazi kwamba tuna mitazamo tofauti. Sisi tunaamini kwamba Wapalestina wana kila haki ya kuishi katika nchi huru, yenye amani na usalama na Rais Biden na jopo lake wataendelea kulifanyia kazi jambo hilo."

Soma pia: Blinken asema Israel inahitaji kuisaidia mamlaka ya Palestina

Mbali ya suala la kuundwa taifa la Palestina, Netanyahu amesema kamwe hawatositisha mashambulizi yao hadi watakapofikia malengo yao ya "ushindi kamili" wa  kuliangamiza kundi la Hamas huko Gaza. Alikuwa akijibu kauli za wakosoaji wanaosema malengo hayo ya Israel kamwe hayawezi kufikiwa huko Gaza.

Israel yaendeleza mashambulizi kusini mwa Gaza

Milio ya risasi na mashambulizi ya anga yameripotiwa mapema leo huko Khan Yunis, ambao ni mji mkubwa kuliko yote kusini mwa Ukanda wa Gaza. Israel inasema eneo hilo limekuwa maficho ya wanachama na viongozi wengi wa vuguvugu la Kiislamu la Palestina la Hamas.      

Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limeripoti mashambulizi makali ya makombora karibu na hospitali ya Al-Amal,  huku wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas ikieleza kuwa watu 77 wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa usiku wa kuamkia leo.

Mwanamke wa Kipalestina akiwa analia baada ya mashambulizi ya Israel katika kambi ya wakimbizi huko Khan Younis kwenye Ukanda wa Gaza: 07.12.2023Picha: Mohammed Dahman/AP Photo/picture alliance

Wizara hiyo imesema pia kuwa zaidi ya Wapalestina 24,620 wameuawa tangu kuanza kwa vita hivyo huku asilimia 70 ya idadi hiyo wakiwa ni wanawake na watoto. Hamas imeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani na mataifa kadhaa ya Magharibi kama kundi la kigaidi.

Soma pia: UN: Hali katika hospitali za Gaza ni mbaya mno

Aidha, magonjwa mbalimbali yameenea huko Gaza huku mashirika ya Umoja wa Mataifa yakionya kuhusu upatikanaji haraka wa misaada ya kiutu. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema limeorodhesha visa 24 vya homa ya ini na maelfu ya visa vya homa ya manjano.

Umoja wa Mataifa unasema vita vilivyoanza na mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, vimesababisha takriban asilimia 85 ya watu milioni 2.4 wa Gaza kuwa wakimbizi. Wengi wao wamejazana kwenye makazi duni na wanatatizika kupata chakula, maji, mafuta na huduma za matibabu.

(Vyanzo: Mashirika)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW