1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yaua makumi katika mashambulizi ya Palestina

11 Septemba 2024

Mashambulizi ya Israel katika maeneo ya Wapalestina yamewaua zaidi ya watu 20 Jumatano. Hayo ni kulingana na maafisa wa mamlaka ya Wapalestina ambao wameongeza kuwa watoto na wanawake ni miongoni mwa waliouawa.

Shambulizi la Israel katika hema yawaua Wapalestina kadhaa
Wizara ya Afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas yasema Wapalestina zaidi ya 40, 000 wameuawa tangu vita vya Gaza vilipoanzaPicha: Jehad Alshrafi/Anadolu/picture alliance

Wizara ya Afya ya Gaza inayosimamiwa na wanamgambo wa Hamas imesema shambulizi la ndege lililofanywa na Israel katika Ukingo wa Magharibi siku ya Jumatano limewaua Wapalestina watano kwenye eneo hilo. Aidha, maafisa wameongeza kuwa watu wasiopungua 20 wakiwemo watoto na wanawake 16 wameuawa katika Ukanda wa Gaza.

Kuhusu shambulizi la Jumanne, wizara ya Afya imesema kambi ya wahamiaji iliyoko eneo ambalo limetengwa mahsusi kwa huduma za kiutu liliwaua watu 19. Wizara hiyo imekadiria kuwa zaidi ya Wapalestina 40,000 wameuawa Gaza tangu vita vya Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas vilipoanza. Hata hivyo, wizara hiyo haitofautishi vifo vya wanamgambo na vya raia kwenye takwimu zake.

Vita hivyo vimesababisha uharibifu mkubwa na kulazimisha asilimia 90 ya wakaazi milioni 2.3 wa Gaza kuwa wakimbizi wa mara kwa mara.

Soma pia: Borrell: Vita vya Gaza ni "janga"

Mnamo Oktoba 7, wanamgambo wa Hamas walishambulia kusini mwa Israel na kuwaua watu 1,200 wengi wakiwa raia. Aidha, watu 250 walishikwa mateka na hadi sasa zaidi ya mateka 100 wangali wanashikiliwa na wanamgambo, ambapo theluthi moja kati yao wanaaminiwa kufariki. Shambulizi hilo ndilo lilichochea vita hivyo.

Soma pia: Israel yaanzisha operesheni kali Ukingo wa Magharibi

Sehemu ya makaazi ya walowezi Ukingo wa MagharibiPicha: Tania Kraemer/DW

Rais wa Israel Isaac Herzog amesema "asubuhi ya leo Jumatano ilikuwa ya huzuni kubwa kwa Waisraeli kwa sababu ya shambulizi la lori la kubeba mafuta katika eneo linalokaliwa na walowezi wa Kiyahudi huko Ukingo wa Magharibi na vilevile ajali ya helikopta iliyoanguka Gaza".

Soma pia: Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani aanza ziara Mashariki ya Kati

Akizungumza akiwa mji mkuu wa Serbia, Belgrade, Herzog alielezea shambulizi la Jumatano kuwa la ‘kusikitisha na kwamba ni tukio la kigaidi'.

Kwingineko, Rais wa Marekani Joe Biden asema "ameghadhabishwa na kusikitishwa mno” kufuatia kifo cha mwanaharakati wa Marekani aliyepigwa risasi na wanajeshi wa Israel alipokuwa akiandamana kupinga ukaliaji wa kimabavu katika Ukingo wa Magharibi, na kukiita kuwa kitendo kisichofaa. Kupitia taarifa amesema sharti kuwe na uwajibikaji kamili na kwamba ni sharti Israel ichukue hatua zaidi kuhakikisha matukio kama hayo hayatokei siku za usoni. 

Soma pia: Biden aahidi kuilinda Israel na vitisho vyote kutoka Iran

Katika tukio tofauti, Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, ameipongeza Misri kwa juhudi zake za upatanishi wa kumaliza vita vya Gaza.

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier (Kushoto) aipongeza Misri kwa juhudi zake za upatanishi kutafuta amani kati ya israel na HamasPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Katika taarifa ya pamoja na Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi mjini Cairo, Steinmeier alihimiza juhudi zaidi kuwezesha mapatano ya usitishaji vita kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas.

Taarifa hiyo ilielezea wasiwasi kwamba kuna hatari ya mzozo huo kutanuka zaidi katika kanda hiyo.

Steinmeier amesema Ujerumani inafanya kila iwezalo na inatambua juhudi za Misri.

Al-Sisi kwa upande wake ameitaka Ulaya kuishinikiza Israel ili kufikia makubaliano ya usitishaji vita.

Soma pia: Vita Gaza ni mtaji wa kisiasa kwa watalawala wa kikanda?

Hayo yakijiri, shirika la Umoja la Mataifa kwa Wapalestina UNRWA, limesema hadi sasa takriban watoto 530,000 wamepokea chanjo dhidi ya ugonjwa wa kupooza katika Ukanda wa Gaza.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW