1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaufungua tena mpaka wake na Gaza

28 Septemba 2023

Israel imeufunguwa tena mpaka wake na Ukanda wa Gaza kuwaruhusu maelfu ya wafanyakazi wa Kipalestina kuingia kwenye nchi hiyo pamoja na Ukingo wa Magharibi wiki moja baada ya kuufunga.

Gaza | Palästinensische Arbeiter am Grenzübergang zu Israel
Picha: Majdi Fathi/NurPhoto/picture alliance

Mpaka huo umefuguliwa tena leo baada ya wiki kadhaa za machafuko, ambapo waandamanaji wenye hasira katika upande wa Gaza walikabiliana na vyombo vya usalama kwa kurusha vifaa vya miripuko na mawe na kurusha maputo yenye moto. 

Israel kwa upande wake ilitumia ndege kufanya mashambulizi kwenye Ukanda huo ikidai kuwa ilikuwa inalenga vituo vya kijeshi vya kundi la Hamas linalotawala ukanda huo.

Kufunguliwa kwa kivuuko hicho kunatokana na juhudi za kimataifa zikiongozwa na Misri na Umoja wa Mataifa zinazodhamiria kutuliza hali ya mambo na kuzuwia awamu mpya ya mapigano kwenye Ukanda wa Gaza.

Soma zaidi: Hujuma za Israel huko Gaza zasababisha vifo vya watu 13

Cogat, ambalo ni baraza maalum ndani ya wizara ya ulinzi wa Israel lenye jukumu la masuala ya kiraia ya Palestina, lilisema jioni ya Jumatano (Septemba 27) kwamba mpaka huo ungefunguliwa leo na utaendelea kubakia wazi madhali tu hali ni tulivu. 

Mapema siku ya Alkhamis (Septemba 28), misururu ya wafanyakazi imeshuhudiwa ikijipanga kukaguliwa kabla ya kuruhusiwa kuuvuka mpaka huo wa Erez, njia pekee kwa Wapalestina wapatao 180,000 wanaotembea kwa miguu kutoka pwani ya Gaza kuingia Israel.

Wafanyakazi hao huingiza wastani wa dola milioni mbili kwa siku kwenye uchumi wa eneo hilo kila wanaporuhusiwa kufanya kazi.

Mzingiro wa umasikini, mzingiro wa ulinzi

Wapalestina waliodumazwa kwa umasikini na mashambulizi ya mara kwa mara wanalazimika kusaka ajira ndani ya Israel, ambako hulipwa mara kumi zaidi ya ilivyo kwenye Ukanda wa Gaza, ambao umezingirwa na Israel na Misri tangu mwaka 2007. Kiwango cha ukosefu wa ajira katika ukanda huo kinakaribia asilimia 50.

Mwanamke wa Kipalestina akivuuka kwenye kivuuko cha Erez.Picha: AP

Israel inadai mzingiro huo unahitajika ili kulizuwia kundi la Hamas kujipatia silaha, lakini wachambuzi wanasema mzingiro huo umeuuwa kabisa uchumi wa Gaza na kuyafanya maisha ya zaidi ya Wapalestina milioni mbili wanaoshi kwenye ukanda huo kuzidi kuwa magumu.

Soma zaidi: UN: Hali inazidi kuwa mbaya Ukanda wa Gaza

Katika miaka ya karibuni, Israel imeanza kutowa vibali vya kazi kusaidia kurejesha utulivu, lakini maafisa wake wanasema vibali hivyo vinakwendana na hali ya usalama.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Israel ilikifunga kwa muda kivuuko kikuu cha mizigo ikidai kwamba ilikuwa imegunduwa mabomu kwenye shehena ya nguo iliyokuwa ikiingizwa Gaza.

Haijulikani kivuuko cha Erez kitasalia wazi kwa muda gani, kwani mapumziko ya wiki moja ya jamii ya Kiyahudi yanaanza kesho Ijumaa, na kawaida Israel huwa inafunga vivuuko vyote wakati wa mapumziko.

Vyanzo: Reuters, AP
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW