Israel yaukubali mpango wa Misri Gaza
15 Julai 2014Uamuzi huo wa baraza la mawaziri la Israel ulitolewa dakika chache kabla ya kuanza kwa usitishwaji wa mapigano majira ya saa 12 Alfajiri. Lakini utulivu uliyofuatia usitishwaji huo ulidumu kwa muda mfupi tu, huku jeshi la Israel likithibitisha kufyetuliwa kwa maroketi matatu kusini mwa Israel kutoka Gaza, ingawa hakukuripotiwa majibu ya mara moja ya kijeshi.
Mapendekezo ya makubaliano ya kusitishwa uhasama, yaliyotolewa na serikali mjini Cairo jana Jumatatu, yaliungwa mkono na utawala mjini Washington wakati ambapo idadi ya vifo mjini Gaza ikifikia 192 kufuatia wiki nzima ya mfululizo wa mashambulizi ya jeshi la anga la Israel.
'Mpango hauna mashiko'
Lakini kundi la Hamas, ambalo wapiganaji wake wamefyetua maroketi zaidi ya 1,000 ndani ya Israel, limesema mpango wa Misri haukuwa na mashiko ingawa halikufunga kabisaa milango ya majadiliano.
Hamas inaonekana kutaka masharti bora zaidi ya usitishwaji mapigano, huku maafisa wa juu wakisema mapendekezo ya sasa hayatoi manufaa ya kueleweka, hasa kuhusu kulegeza vizuiwi ilivyowekewa Gaza na Israel na Misri.
Hamas pia inataka kutambuliwa na Misri kama mshirika katika juhudi zozote za kufikia makubaliano. Afisa mwandamizi wa kundi hilo mjini Gaza, Sami Abu Zuhri, amesema Misri haikushauriana nao.
Misri ilitoa mapendekezo hayo baada ya Marekani kuionya Israel dhidi ya kufanya mashambulizi ya ardhini, lakini ikashindwa kulaani ongezeko la mauaji ya raia wa Palestina wasio na hatia, na kuitaka Hamas kuacha kufyatua roketi ndani ya Israel.
Netanyahu atishia mashambulizi makali zaidi
Waziri mkuu Benjamini Netanyahu alisema Israel inayaona mapendekezo hayo kama fursa ya kuondoa mambo ya kijeshi katika ukanda wa Gaza, lakini ameongeza kuwa ikiwa Hamas haikubaliani na mapendekezo hayo kama inavyoonekana sasa, Israel itakuwa na uhalali wote wa kisheria kutanua operesheni yake ya kijeshi ili kupata utulivu unaotakiwa.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, aliekuwa mjini Tel Aviv amezitaka pande husika kuyakubali mapendekezo ya Misri, huku akisisitiza urafiki baina ya Ujerumani na Israel, na kusema nchi hiyo ina haki ya kimataifa, kisiasa na kimaadili ya kujilinda.
Wakati huo huo, waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ameituhumu Israel kwa kufanya ugaidi wa dola dhidi ya ukanda wa Gaza. Erdogan amewambia wabunge wa chama chake tawala kuwa dunia nzima imefumbia macho ugaidi huu wa Israel, na kuhoji hadi lini jamii ya kimataifa itaendelea na ukimya huo.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape,afpe
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman