1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yauwa wanajeshi, wanamgambo 11 wa Syria

9 Juni 2021

Wanajeshi na wanamgambo 11 wa Syria wameuawa baada ya ndege za Israel kushambulia maeneo ya kati na kusini mwa nchi hiyo, sehemu ya mashambulizi yake ya kila mara kwa madai ya kuzuwia ushawishi wa Iran.

Israel Golan-Höhen Panzer-Manöver
Picha: JALAA MAREY/AFP/Getty Images

Mashambulizi hayo yaliyofanyika muda mchache kabla ya saa 6:00 usiku wa Jumanne (Juni 8) yalivilenga vituo vya kijeshi kwenye kijiji cha Khirbet al-Tin kilicho maeneo ya mashambani ya jimbo la Homs.

Kwa mujibu wa Shirika la Ufuatiliaji wa Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake nchini Uingereza, waliouawa ni pamoja na wanajeshi wa kikosi maalum cha wanamgambo wanaoiunga serikali kiitwacho "Ulinzi wa Taifa." 

Shirika hilo lilisema kuwa ghala la silaha linaloaminika kumilikiwa na wanajeshi wa Hizbullah wa Lebanon lilishambuliwa pia kwenye hujuma hiyo ya jeshi la Israel.

Mripuko ulisikika pia kwenye Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa Dabaa. 

Taarifa za mashambulizi hayo zilithibitishwa pia na shirika rasmi la habari la Syria, SANA, ambalo lilisema kuwa ndege za kijeshi za Syria zilishambulia maeneo kadhaa ndani ya Syria usiku wa Jumanne.

Shirika hilo lilinukuu vyanzo vya kijeshi vikisema kuwa maroketi yalipiga maeneo ya kati na kusini, ingawa halikufafanuwa madhara yake.

Israel yatumia anga ya Lebanon kushambulia Syria

Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha usalama nchini Lebanon, ndege za Israel zilitumia anga la Lebanon kushambulia maeneo ya kusini mwa mji mkuu wa Syria, Damascus. 

Maroketi ya Israel yakirushwa kuelekea mji mkuu wa Syria, Damascus.Picha: Ammar Safarjalani/Xinhua/picture alliance

Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu lilithibitisha kuwa mshindo mkubwa ulisikika kwenye viunga vya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Damascus na pia kwenye kambi ya wanajeshi wa anga karibu na eneo hilo katika mkoa wa Dmeir.

Miripuko ilisikika pia kwenye majimbo ya Hama na Latakia. 

Hadi sasa, hakuna taarifa yoyote kutoka Israel, ambayo daima imekuwa ikidai kuwa kuishambulia kwake Syria ni kwa ajili ya kuizuwia Iran, mmoja wa washirika muhimu wa utawala wa Rais Bashar al Assad wa Syria, isiimarishe ushawishi wake wa kijeshi kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati.

Tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vianze nchini Syria mwaka 2011, Israel imeshafanya mashambulizi zaidi ya mia moja ndani ya ardhi ya Syria, ikivilenga vikosi vya jeshi la Syria, vya Iran na vya wanamgambo wa Hizbullah kutoka Lebanon, ambavyo vinaisaidia serikali ya Assad.

Utawala wa Israel umeapa kwamba kamwe hautaliwacha taifa jirani la Syria kuwa kituo cha mashambulizi cha hasimu wake mkuu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, taifa lisilotambuwa uhalali wa dola la Kiyahudi la Israel.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW