1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaamuru raia 100,000 kuondoka Rafah

6 Mei 2024

Jeshi la Israel limewaamuru maelfu ya watu kuondoka katika mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah, hii ikiashiria kuwa operesheni ya kijeshi iliyokuwa ikitajwa kwa muda mrefu huenda inakaribia kuanzishwa.

Gaza | Baadhi ya Wapalestina wakianza kuondoka Rafah
Baadhi ya Wapalestina wakianza kuondoka Rafah kufuatia agizo la Jeshi la Israel: 06.05.2024Picha: Hatem Khaled/REUTERS

Tangazo hilo la Israel limekwamisha juhudi za hivi punde za wapatanishi wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Marekani, Qatar na Misri za kutafuta  kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano  huko Gaza . Viongozi wa Kundi la Hamas pamoja na maafisa wa Qatar ambao ndiyo wapatanishi wakuu, wameonya kuwa uvamizi wa Rafah unaweza kuharibu mchakato wa mazungumzo ya kusaka makubaliano ya usitishwaji mapigano.

Mazungumzo hayo yaliondelea hadi usiku wa jana mjini Cairo nchini Misri yameshindwa kufikia muafaka kutokana na misimamo isiyotetereka ya pande zote. Hamas imesema kamwe haitoafiki makubaliano yoyote ambayo hayatohusisha usitishwaji kamili wa vita na kuondoka kabisa kwa vikosi vya Israel katika ardhi ya Palestina, jambo ambalo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema hawawezi kamwe kukubaliana nalo.

Baadhi ya Wapalestina wakianza kuondoka Rafah kufuatia amri ya Jeshi la Israel: 06.05.2024Picha: Hatem Khaled/REUTERS

Wakati baadhi ya Wapalestina  wakianza kuondoka Rafah , usiku wa kuamkia leo, Israel imefanya mashambulizi ya anga huko Rafah na kuwaua watu wasiopungua 22 wakiwemo wanawake sita na watoto watano. Rasha Qishta, ni jamaa wa waliouawa katika shambulio hilo.

" Mtoto huyu mchanga, baba na mama yake waliuawa kama mashahidi huko Tal al-Sultan mjini Rafah. Ndege ya Israel ilifyetua bomu kwenye nyumba yao. Kaka yangu na mke wake waliuawa mara moja, na mtoto wao akabaki hai. Mama yake alikuwa na ujauzito wa miezi minane na madaktari walimwokoa mtoto huyu dakika za mwisho. Alizaliwa na mama yake aliuawa, baadaye walihamia kwenye nyumba ya babu yao ambayo pia ilishambuliwa na mtoto huyu kuuawa kama shahidi. Dada zake wawili bado wapo huko na hatujui hali zao kwa maana bado wapo chini ya vifusi."

Malengo ya Israel katika kuishambulia Rafah

Baada ya miezi saba ya vita, Israel imekuwa ikidai Rafah ndiyo ngome kuu ya mwisho ya Hamas na viongozi wake akiwemo waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wamekuwa wakielezea mara kwa mara haja yao ya kuanzisha operesheni ya ardhini ili kuliangamiza kabisa kundi la Hamas ambalo limeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa kadhaa ya Magharibi kuwa kundi la kigaidi.

Msemaji wa Jeshi la Israel la Ulinzi la Israel (IDF)- Daniel HagariPicha: dts Nachrichtenagentur/IMAGO

Luteni Kanali Nadav Shoshani, miongoni mwa wasemaji wa jeshi la Israel, amesema kuwa takriban watu 100,000 waliamriwa kuhamia katika kambi inayoitwa Muwasi ambako Israel imewasilisha misaada ya kibinaadamu ikiwa ni pamoja na vituo vya afya, mahema, chakula na maji.

Soma pia: Israel yaanza kuwahamisha raia 100,000 kutoka Rafah

Askari huyo amesema Israel ilikuwa ikijiandaa kuanzisha "operesheni ndogo katika eneo rasmi", bila hata hivyo kuelezea ikiwa ndio mwanzo wa uvamizi kamili wa jiji la Rafah. Hatua hii inajiri siku moja baada ya wanamgambo wa Hamas kufanya shambulio la roketi kutoka eneo hilo na kuwaua wanajeshi watatu wa Israel.

Katika kuendeleza juhudi za kidiplomasia, Rais wa Marekani Joe Biden atakutana kwa mazungumzo katika Ikulu ya White House na mshirika wake wa Mashariki ya Kati, Mfalme Abdullah II wa Jordan, katika matarajio ya kusaka makubaliano ya usitishaji mapigano huko Gaza.

(Vyanzo: Mashirika)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW