Israel yashambulia tena Hezbollah, Iran ikiitishia Marekani
5 Machi 2026
Kulingana na ujumbe ulioandikwa na jeshi la anga la Israel katika mtandao wa kijamii wa X, mashambulizi hayo yamelenga miundo mbinu iliyotumiwa na wanamgambo hao.
Vyombo vya habari mjini Beirut pia vimeripoti mashambulizi kusini mwa mji huo mkuu katika kambi moja ya wakimbizi wa Palestina ambapo watu wawili wameuwawa na mmoja kujeruhiwa.
Haya yanafanyika wakati ambapo Iran leo imekanusha madai kwamba imerusha kombora la masafa marefu kuelekea Uturuki ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Mkuu wa Utumishi wa Jeshi la Iran amesema madai hayo ya Uturuki ni ya uongo na hawayakubali. Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Iran ameitishia Marekani baada ya kuizamisha meli yake ya kijeshi katika Bahari Hindi.
Iran imesema tukio hilo ni ukatili. Zaidi ya watu 80 walifariki dunia kufuatia kuzamishwa kwa meli hiyo.