1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiIsrael

Israel yawashikilia wafungwa zaidi ya 1,200 bila mashtaka

Sylvia Mwehozi
2 Agosti 2023

Shirika moja la haki za binadamu la Israel, limesema kuwa nchi hiyo inawashikilia zaidi ya wafungwa 1,200 bila ya kuwafungulia mashtaka huku wengi wao wakiwa ni Wapalestina.

Israel  Jenin
Askari wa Israel wakiwa wakilinda uzio katika Ukingo wa MagharibiPicha: Ilia Yefimovich/dpa/picture alliance

Wafungwa hao ambao asilimia 99 ni Wapalestina, wanashikiliwa chini ya sera ya Israel ya "vizuizi vya kiutawala" bila ya kufunguliwa mashitaka na chini ya madai ambayo mamlaka ya nchi hiyo inafanya siri. Kwa mujibu wa Shirika la haki za binadamu la Hamoked la nchini Isreal, ambalo limechapisha takwimu hizo, ni kwamba vifungo hivyo vinatofautiana kuanzia miezi hadi miaka na mamlaka zinaweza kurefusha adhabu hizo bila sababu zinazojulikana.Israel yapeleka polisi wengi eneo la maandamano

Mkurugenzi wa shirika hilo Jessica Montell, amesema kuwa viwango hivyo vya juu vinachukiza na kutoa wito kwa wafungwa kushitakiwa kwa haki au kuachiliwa huru.  Montell ameongeza kuwa licha ya kwamba amri ya watu kuzuiliwa imepangwa kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita, lakini kwa wastani wafungwa nchini humo huzuiliwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Israel inadai kwamba mbinu hizo zenye utata ni muhimu katika kudhibiti wanamgambo hatari na kuepuka kufichua taarifa za kuwatia hatiani kwa sababu za kiusalama. Lakini Wapalestina na makundi ya haki za binadamu yanasema mfumo huo unatumiwa vibaya.

Watu wakikimbia mapigano katika kambi ya wakimbizi JeninPicha: Jaafar Ashtiyeh/AFP/Getty Images

Idadi ya wafungwa chini ya sera hiyo imeongezeka mara mbili tangu mapema mwaka jana, wakati Israel ilipoanza uvamizi wa usiku kwenye miji ya Kipalestina kufuatia mashambulizi ya Wapalestina. Shirika hilo linasema kuwa sera hiyo ya uzuiaji hata hivyo inatumiwa mara chache dhidi ya Wayahudi au Waisreali lakini idadi imeongezeka ambapo Waisrael 14 walizuiliwa kufikia mwezi Machi.

Israel na wanamgambo wa Kipalestina warushiana makombora GazaSio shirika la usalama la Israel ya Shin Bet, wala jeshi ambalo lilitoa maoni mara moja kuhusu takwimu hizo za wafungwa wa sera ya kiutawala. Israel inasema kwamba shughuli zake katika maeneo yanayokaliwa ya Ukingo wa Magharibi zinalenga kuzuia mashambulizi. Mwaka mmoja na nusu uliopita umeshuhudia umwagikaji damu mkubwa katika eneo hilo katika kipindi cha karibu miongo miwili. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la habari la Associated Press, zaidi ya Wapalestina 160 wameuawa katika mapigano ya mwaka huu.

Kulingana na Israel, wahanga wengi waliokufa walikuwa ni wanamgambo. Lakini watano kati yao walikuwa watoto chini ya umri wa miaka 14. Waziri wa usalama wa mambo ya ndani mwenye msimamo mkali Itamar Ben-Gvir, amekuwa akihimiza hatua kali dhidi ya wafungwa wa Kipalestina walioko jela za Israel. Ukingo wa Magharibi umekuwa chini ya udhibiti wa jeshi la Israel tangu nchi hiyo ilipolitwaa eneo hilo katika vita ya Mashariki ya Kati ya mwaka 1967. Wapalestina wanalitaka eneo hilo ili kuunda sehemu kubwa ya taifa lao lijalo.

Chanzo: AP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW