1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel yawataka wakaazi kusini mwa Lebanon kuondoka

Hawa Bihoga
23 Septemba 2024

Jeshi la Israel limewataka wakaazi wa kusini mwa Lebanon kuyahama makaazi yao mara moja kutokana na kile ilichokisema yanatumiwa na kundi la Hezbollah kuhifadhi silaha na kusema "itafanya mashambulizi makali."

Israel, Kiryat Bialik | Jeshi likizima moto baada ya shambulio kutoka Lebnon.
Vikosi vya uokoaji vya Israel vikizima moto baada ya shambulio la Hezbollah kaskazini mwa Israel.Picha: Gil Nechushtan/AP Photo/picture alliance

Indhari hiyo kutoka jeshi la Israel ni ya kwanza na ya aina yake katika kipindi cha takriban mwaka mmoja wa mzozo unaozidi kuongezeka katika eneo hilo la Mashariki ya Kati. Imetolewa baada ya majibizano makali ya mashambulizi kutoka pande zote za mzozo hapo jana Jumapili.

Hezbollah ilivurumisha  takriban makombora 150 pamoja na droni kuelekea kaskazini mwa Israel ikiwa ni mashambulizi ya kulipiza kisasi baada ya kuuliwa kwa kamanda wake pamoja na wapiganaji wengine.

Vyombo vya habari vya Lebanon vimeripoti kuwa wakaazi katika eneo hilo wamepokea ujumbe wa maandishi wakihimizwa kuondoka katika majengo ambayo Hezbollah huyatumia katika kuhifadhi silaha.

Soma pia:Israel yaanzisha mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon

Msemaji wa Jeshi la Israel Daniel Hagari amesema kwa zaidi ya kipindi cha miaka 20 kundi hilo limekuwa likitumia makaazi ya raia kuficha silaha zake na lengo la oparesheni hiyo ni kuziteketeza silaha hizo.

"Hiki ni kijiji cha kusini mwa Lebanon. Hezbollah wanahifadhi makombora, roketi, silaha ya kufyatulia makombora ndani ya nyumba za raia."

Aliongeza kwamba katika oparesheni ambayo wamepanga kuifanya italenga kuzisaka na kuziharibu silaha zote.

Haikuweza kubainika hasa ni watu wangapi ambao wameathirika na amri hiyo ya Israel. Idadi kubwa ya jamii zinazoishi maeneo ya mpakani zimehamishwa kutokana na kushuhudiwa kwa mashambulizi ya mara kwa mara.

Israel: Tutaendeleza mashambulizi Lebanon

Waziri wa Ulinzi Israel Yoav Gallant amesema wataendeleza na mbinyo wa mashambulizi nchini Lebanon hadi pale watakapotimiza malengo yao na kuhimiza utulivu ndani ya Israel katika wakati huu.

Kuongezeka kwa majibizano ya mashambulizi kutoka kila upande kumeongeza hofu ya kutanuka kwa mzozo huo katika wakati huu ambapo jeshi la Israel bado linapambana na kundi la Hamas huko Gaza, ikijaribu kuwarejesha mateka waliochukuliwa baada ya shambulio la mnamo Oktoba 7. Hezbollah imeapa kuendelea mashambulizi yake iliyoyataja yakuonesha mshikamano kwa Wapalestina na Hamas.

Shambulizi la roketi lauwa watu 12 katika milima ya Golan

01:03

This browser does not support the video element.

Soma pia:UN yaonya juu ya janga kubwa katika kanda ya Mashariki ya Kati

Kikosi cha kulinda amani cha UNIFIL kusini mwa Lebanon kupitia kwa msemaji wake Andrea Tenenti amesema kumekuwa na ongezeko la mashambulizi ya mabomu katika eneo lote la oparesheni hasa katika eneo la mpaka wa Israel na Lebanon.

Mashambulizi haya yanafanyika huku kukiwa na mapigano makali zaidi kwa takriban mwaka mmoja wa mzozo unaoendelea kusambaa na vita kati ya Israel na Hamas huko Gaza.

Kando na Lebanon, mashambulizi makubwa ya vikosi vya Israel katika moja ya kambi ya wakimbizi yamesababisha vifo vya Wapalestina kumi wakiwemo watoto wanne katika eneo la Ukanda wa Gaza hii leo.

Mashambulizi hayo yanafanyika katika wakati ambapo nadhari ya kimataifa imeugeukia mzozo wa Lebanano kati ya Israel na kundi la Hezbollah.