1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yazidi kushinikizwa kusitisha mapigano Gaza

26 Januari 2024

Wasiwasi unazidi kuongezeka kwa raia waliozingirwa na mapigano kote katika jiji la Khan Younis katikati ya ongezeko la miito ya kimataifa kuhusiana na hali tete inayowakabili raia wanaoishi kwenye eneo hilo.

Moto waunguza jengo la UNRWA baada ya kushambuliwa
Raia wa Palestina wakijaribu kuzima moto katika jengo la shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina UNRWA, kufuatia shambulizi la IsraelPicha: Ramez Habboub/AP Photo/picture alliance

Hali ni mbaya sio tu katika jiji la Khan Younis ambalo ni kubwa zaidi kusini mwa Gaza, lakini pia kwenye maeneo mengine ya ukanda huo. Kulingana na Wizara ya Afya inayosimamiwa na kundi la Hamas, karibu watu 26,083 wameuawa katika vita kati ya kundi hilo na Israel.

Taarifa za mapema leo kutoka Wizara hiyo ya afya zimesema watu 20 waliuawa na wengine 150 kujeruhiwa walipokuwa wakisubiri kugawiwa misaada ya kiutu katika viunga vya kaskazini mwa Jiji la Gaza.

Abu Ata Basal, mjomba wa miongoni mwa majeruhi aliliambia shirika la habari la AFP kwamba "watu walikuwa wakisubiri kupewa chakula na unga kwa sababu hawakuwa na chochote cha kula." Lakini ghafla, vifaru vikatokea na kuanza kuwafyatulia watu risasi, na miili ya wengine ilikatika vipande vipande, aliongeza.

Soma pia: Israel yazidisha mashambulizi baada ya askari wake kuuawa

Mwandishi wa habari wa AFP alisema alishuhudia miili ikiwa imetapakaa sakafuni katika hospitali ya al-Shifa. Hamas wamesema tukio hilo ni sawa na "uhalifu wa kutisha wa kivita", ambalo kulingana na kundi la wanamgambo wa Palestina la Islamic Jihad wanasema lilisababishwa na mashmabulizi ya risasi na makombora.

Daktari akiwatibu raia wa Palestina waliojeruhiwa baada ya shambulizi la angani lililofanywa na Israel katika jiji la Khan YounisPicha: Hatem Ali/AP Photo/picture alliance

Israel haijasema chochote kuhusiana na madai hayo na AFP yenyewe haikuweza kuyathibitisha. Shambulizi hilo limefanyika siku moja baada ya Umoja wa Mataifa kusema vifaru vilishambulia makazi yake yaliyopo huko Khan Younis na kuwaua watu 13.

Ufaransa imeomba Israel kuheshimu sheria za kimataifa na kuunga na Marekani katika kulaani shambulizi hilo la Khan Younis, ingawa haikumtamja moja kwa moja Israel kama muhusika.

Soma pia: Israel yaendelea kuitwanga Khan Younis

Uingereza yaelezea mashaka juu ya hali ya kiutu, Gaza

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak pia ameelezea wasiwasi wake kuhusiana na kitisho dhidi ya maisha ya watu wa Gaza baada ya kituo cha utangazaji cha ITV kurusha picha zilizoonyesha raia aliyeshambuliwa licha ya kuwa na bendera nyeupe mkononi na kurudia tena kutoa wito kwa Israel na Hamas kusitisha mapigano, kuwaachia mateka na kuruhusu upitishwaji wa misaada ya kibinaadamu.

"Unajua, Rais Biden alizungumza na mimi kuhusu hili mapema wiki hii. Nimezungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusu hili. Na kile tunachotaka kukiona ni kusimamishwa mapigano ili mateka waachiwe na misaada zaidi kuingizwa kwenye Ukanda wa Gaza." 

Hamas aidha imeripoti mashambulizi makali katikati ya magharibi mwa mji wa Khan Younis, ambako kuna makazi ya mkuu wa kundi hilo Yahya Sinwar.

Na kutoka huko Washington, taarifa zinasema mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la nchini Marekani, CIA atakutana na wenzake kutoka Israel na Misri pamoja na Waziri Mkuu wa Qatar ili kufanya mazungumzo ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka wa vita hivyo, hii ikiwa ni kulingana na vyombo vya habari vya Marekani jana Alhamisi.

William Burns atakutana na wakuu hao wengine katika siku chache zijazo, limearifu Washington Post na Axios, ingawa havikutaja mahali watakapokutana. Hata hivyo, si CIA yenyewe wala Ikulu ya White House waliokubali kuthibitisha taarifa hizi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW