Israel yazidi kusogea katika maeneo ya Gaza
30 Oktoba 2023Vikosi na vifaru vya Israel vimesogea zaidi kuelekea Gaza haswa katika maeneo mawili makuu ya mji huo. Video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii imeonesha kifaru cha Israel na tingatinga katikati mwa Gaza vikizuia barabara kuu inayounganisha eneo la Kaskazini Kusini, ambayo hapo awali jeshi la Israel lilikuwa limewaeleza Wapalestina kuitumia kukwepa mashambulizi yanayoongezeka ya ardhini.
Makumi kwa maelfu ya Wapalestina ambao wamesalia upande wa Kaskazini hawatakuwa na uwezo wa kukimbia kama barabara hiyo itazuiwa kwakuwa ndio njia pekee ya kuelekea kusini. Kusonga mbele kwa Israel kunaviweka vikosi vyake katika pande zote za mji wa Gaza na maeneo ya karibu ya kaskazini, katika kile ambacho Waziri Mkuu Netanyahu amekitaja kuwa ni "awamu ya pili" ya vita vilivyochochewa na shambulizi la kikatili la Hamas la Okotoba 7.
Hayo yakijrii, kundi la Hamas limetoa mkanda wa video unaowaonyesha wanawake watatu waliochukuliwa mateka wakati wa shambulizi lake la Oktoba 7 ndani ya Israel. Katika mkanda huo uliotolewa leo na kundi la Hamas, mwanamke mmoja kati ya wanawake hao watatu amesikika akitoa taarifa fupi na kuzikosoa mamlaka za Israel kwa namna zinavyoshughulikia mzozo wa kuwakomboa mateka.
Mateka walioachiliwa: Mateka wawili waachiwa huru na kundi la Hamas
Haikuwezekana mara moja kuthibitisha utambulisho wa mwanamke huyo katika video ya sekunde 76 ambayo amesikika akitoa wito kwa Waziri Mkuu wa Isreal Benjamin Netanyahu wa kufikia makubaliano ya kubadilishana wafungwa ili kuachiliwa mateka wote.
Akizungumza kwa Kiyahudi na akiwa ameketi kwenye kiti cha plastiki, mwanamke huyo ambaye Hamas imemtaja kuwa "mateka wa kizayuni", alionekana kufadhaika sana na kuanza kupiga kelele karibia mwishoni mwa mkanda huo huku wanawake wengine wawili wakiketi kando yake wakiwa kimya.
Kwanini Hamas iliwateka Waisrael: Ni lipi kusudio la Hamas kuwachukua mateka raia wa Israel?
Wanamgambo wa Hamas waliwateka watu takribani 240 wakati wa shambulizi lao la Oktoba 7 na wamedai kwamba watawaachia endapo Israel nayo itawaachia maelefu wa wafungwa wa Kipalestina inaowashikilia.
Na huko katika Ukingo wa Magharibi Mpalestina mmoja amemchoma kisu na kumjeruhi polisi wa Israel katika eneo lililonyakuliwa la jerusalem Mashariki kabla ya kupigwa risasi na polisi wa mpakani. Wapalestina wengine watano wameuawa kwenye Ukingo wa Magharibi kwa mujibu wa wizara ya afya, wanne kati yao ni wakati wa uvamizi wa Israel kaskazini mwa mji wa Jenin na mwingine aameuawa huko Yatta karibu na Hebron upande wa kusini.
Soma pia: Vita vya Israel vyahofiwa kusambaa maeneo mengine
Tangu vita vya Gaza vilipoanza, wizara ya afya ya Palestina imesema kwamba zaidi ya wakaazi 120 wa Ukingo wa Magharibi wameuawa katika uvamizi wa jeshi na mashambulizi dhidi ya Walowezi.
Mapema leo pia jeshi la Israel limedai kushambulia miundombinu ya kijeshi huko Syria baada ya maroketi yaliyofyatuliwa kutokea pande hizo kuanguka katika eneo la wazi la Israel. Waisrael wapatao 250,000 wamehamishwa kutoka kwenye makaazi yao kwasababu ya ghasia za mpakani mwa Gaza na katika mpaka wa Kaskazini na Lebanon kwa mujibu wa jeshi la Israel.