Israel yazidi kulipua Gaza huku wapatanishi wakikutana Cairo
5 Oktoba 2025
Jeshi la Israel limepiga maeneo kadhaa ya Ukanda wa Gaza usiku kucha na Jumapili, likiharibu majengo ya makaazi kadhaa.
Mashambulizi hayo yanakuja wakati Wapalestina waliokata tamaa wakitumaini mpango wa Rais Donald Trump unaweza kumaliza mateso yao.
Trump alitangaza kwamba Israel imekubali "mstari wa awali wa uondoaji" ndani ya Gaza na kwamba pindi Hamas itakapothibitisha, makubaliano ya kusitisha mapigano yataanza mara moja.
Wakati huo huo, Misri inajiandaa kuwapokea wajumbe kutoka Hamas, Israel, Marekani na Qatar kwa mazungumzo ya utekelezaji wa mpango huo wa amani unaotajwa kuwa wa maendeleo zaidi tangu vita kuanza.
Mazungumzo ya Cairo kujadili masuala yasiokamilika
Hamas ilionyesha kukubali vipengele muhimu vya pendekezo la Trump, ikiwemo kumaliza vita, kuondoka kwa Israel na kuachiliwa kwa mateka. Hata hivyo, baadhi ya masuala muhimu kama suala la kuachana na silaha bado hayajakubaliwa.
Mjumbe mmoja wa Kipalestina alisema maendeleo yatategemea kama Hamas itakubali ramani inayowapa wanajeshi wa Israel udhibiti wa sehemu kubwa ya Gaza.
Katika soko la fedha, ishara za matumaini zilijitokeza baada ya tangazo hilo. Sarafu ya shekel ilipanda hadi kiwango cha juu zaidi katika miaka mitatu dhidi ya dola ya Marekani, huku hisa za Tel Aviv zikifikia rekodi mpya.
Lakini ndani ya Israel, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anakabiliwa na shinikizo kali kati ya madai ya umma ya kumaliza vita na mashinikizo kutoka kwa wanasiasa wakali wanaotaka mashambulizi yaendelee.
Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich alionya kwamba kusitisha mashambulizi Gaza kutakuwa "kosa kubwa,” akitishia kuvunja serikali endapo vita vitasitishwa.
Nchi za Kirabu zaunga mkono mpango wa amani
Upinzani wa kisiasa nchini Israel unaoongozwa na Yair Lapid umeahidi kutoa uungwaji mkono wa kisiasa ili mpango wa Trump usivurugwe.
Trump amepata pia uungaji mkono kubwa kutoka kwa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu, ikiwemo Saudi Arabia, Qatar, Misri, Jordan, Uturuki, Indonesia na Pakistan. Nchi hizo zilitangaza kujitolea kusaidia utekelezaji wa mpango huo na kumaliza vita mara moja.
Katika Jiji la Gaza, mashambulizi yameendelea, na jeshi la Israel limeonya wakaazi kutojaribu kurejea katika maeneo waliyoyahama likiyataja kuwa "maeneo hatari ya mapigano.”
Mashuhuda walisema ndege za kivita ziliongeza mashambulizi Jumapili asubuhi, zikipiga maeneo ya Sabra na Sheikh Radwan. Usiku uliopita, mabomu yaliyodondoshwa na droni yaliharibu majengo kadhaa ya makazi.
"Yuko wapi Trump katika haya yote?” aliuliza Rami Mohammad-Ali, mkazi wa Gaza mwenye umri wa miaka 37, akihofia kwamba mpango wa amani huenda usitekelezwe.
Wizara ya Afya ya Gaza imeripoti takribani vifo vya Wapalestina wanne na wengine kadhaa kujeruhiwa, huku uhaba wa chakula na mafuta ukizidi katika jiji hilo lililozingirwa.
Hamas yakubali mabadilishano ya mateka na wafungwa
Chini ya mpango wa Trump, mateka wote wa Israel waliosalia wanatakiwa kuachiliwa ndani ya saa 72 tangu Israel ikubali makubaliano hayo.
Hata hivyo, vyanzo vya Hamas vimesema urejeshaji wa miili ya waliokufa unaweza kuchukua muda kutokana na uharibifu mkubwa uliopo.
Trump amesema anaamini Hamas "iko tayari kwa amani ya kudumu,” akimtaka Netanyahu asitishe mashambulizi.
Vita vilianza Oktoba 7, 2023, baada ya shambulio la Hamas lililosababisha vifo vya watu 1,200, wengi wao raia, na mateka 251.
Mashambulizi ya Israel yamesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 67,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Mazungumzo Cairo yatarajiwa kufafanua mwelekeo mpya
Wajumbe wa Israel na Hamas wanatarajiwa kuanza mazungumzo mjini Cairo kuhusu kusitisha vita na kubadilishana mateka.
Netanyahu amesema matarajio yake ni kwamba mateka wote "watarudishwa nyumbani” kabla ya mwisho wa sikukuu ya Kiyahudi ya Sukkot.
Trump ametuma wajumbe wawili – Jared Kushner na Steve Witkoff – kuongoza jitihada za kidiplomasia na kusimamia maelezo ya mwisho ya mpango huo.
Hamas imesisitiza kuwa itakuwa na nafasi katika utawala wa baada ya vita, jambo ambalo mpango wa Trump unalikataa wazi, ukitaka Gaza isimamiwe na serikali ya mpito ya kiufundi chini ya usimamizi wa kimataifa.
Israel Katz: Wapalestina 900,000 wamehama Gaza
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema mashambulizi katika Gaza City yamesababisha watu takriban 900,000 kuyakimbia makazi yao kuelekea kusini, na hivyo kuongeza shinikizo kwa Hamas.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kabla ya mashambulizi ya mwezi Agosti, watu milioni moja waliishi Gaza City na maeneo ya jirani.
Wakati huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul anazuru mataifa ya Ghuba kujadili mpango wa Trump. Amesema "ushirikiano wa kimataifa thabiti” unahitajika ili kufanikisha amani na kuachilia mateka wote.
Wadephul amepongeza jukumu la Qatar kama mpatanishi muhimu kati ya Israel na Hamas, akisema Ujerumani iko tayari kusaidia katika ujenzi upya na utulivu wa Gaza.
Waziri huyo atakutana na mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya na Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC) nchini Kuwait kujadili mikakati ya muda mrefu ya amani na usalama katika Mashariki ya Kati.
Chanzo: RTRE, AFP, DPA