1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel,Hamas warefusha muda wa usitishaji vita

Angela Mdungu
30 Novemba 2023

Israel na kundi la wanamgambo la Hamas wamekubaliana kurefusha muda wa kusimamisha mapigano kwa siku nyingine moja, muda mfupi kabla ya makubaliano hayo kumaliza muda wake.

Israel Hamas | Kuongezwa muda kwa  usitishaji wa mapigano
Israel na Hamas zimerefusha muda wa usitishaji vita Picha: Mohammed Ali/XinHua/dpa/picture alliance

Baada ya hatua hiyo, Israel imesema kuwa imepokea orodha ya majina ya mateka wengine ambao huenda wakaachiliwa Alhamisi, baada ya makubaliano ya kusimamisha mapigano kuingia katika siku yake ya sita.

Makubaliano mapya ya kusitisha vita kwa siku moja zaidi tayari yamethibitishwa na Israel pamoja na msuluhishi wa mzozo kati ya Hamas na Israel, Qatar. Taarifa ya jeshi la Israel iliyotolewa kupitia mitandao ya kijamii imesema hatua hiyo ya kusitisha mapambano itaendelea kutokana na juhudi za wapatanishi kuendelea na mchakato wa kuwezesha kuachiliwa mateka na kwa kuzingatia masharti ya makubaliano.

Soma zaidi: Wapatanishi waeleza matumaini ya kurefushwa usitishaji mapigano kwa siku mbili zaidi

Qatar na Israel zimesema huenda usitishwaji mapigano ukaendelea chini ya mkakati wa sasa ambapo kundi la Hamas limewaachilia mateka 10 kwa siku kwa sharti la Israel kuwaachilia wafungwa 30 wa Kipalestina.

Tangu kuanza kwa usitishwaji vita Ijumaa iliyopita, kundi la Hamas limeshawaachilia huru mateka 97 wengi wao wakiwa ni Waisrael, wakati Israel nayo imewaachilia wafungwa 210 wa Kipalestina.

Orodha ya wanaotarajiwa kuachiliwa na Hamas yawasilishwa Israel

Baada ya makubaliano hayo, Israel imetangaza kuwa imepokea kutoka kwa kundi la Hamas orodha ya majina ya mateka wengine ambao huenda wakaachiliwa Alhamisi ambao ni wanawake na watoto.

Watoto wa Kipalestina mbele ya majengo yaliyoharibiwa na mashambulizi katika kambi ya wakimbizi ya JebaliyaPicha: Mohammed Hajjar/AP Photo/picture allinance

Hayo yakiendelea, watu watatu wameripotiwa kuuwawa baada ya kupigwa risasi katika kituo kimoja cha basi mjini Jerusalem. Watu wengine sita wamejeruhiwa katika tukio hilo, kulingana na taarifa iliyotolewa na shirika la huduma za dharura la Israel Magen David Adom.

Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken amewasili mjini Tel Aviv hii leo kukutana na viongozi wa Israel. Kati ya yanayotarajiwa kujadiliwa katika ziara yake hiyo ni pamoja na suala la haki ya Israel kujilinda kwa kuzingatia sheria ya kiutu ya kimataifa na kuongeza misaada kwa wakaazi wa Gaza.Hii ni mara ya tatu kwa Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Marekani kuizuru Mashariki ya kati tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na kundi la Hamas.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi