Israeli kuendelea na ujenzi Ukingo wa Magharibi
4 Desemba 2012Wapalestina nao wamekimbilia Umoja wa Mataifa wakiutaka kusitisha ujenzi huo ambao wanauita uchokozi wa Israel.
Israel imesema kuwa itaendelea na ujenzi kwenye eneo la Ukingo wa Magharibi ambalo linaungana na Jerusalem pamoja na sehemu ijulikanayo kama Maáleh Adumin au E-1.
Ujenzi huo hautaugawa tu ukingo wa magharibi katika sehemu mbili, bali pia utawatenga Wapalestina na eneo la mashariki ya Jerusalem ambalo wanalitaka kama mji mkuu wao wa baadae.
Afisa mmoja wa Israel ambaye hakutaka kutajwa jina amenukuliwa na Shirika la Habari la Ujerumani, DPA, akisema kuwa kitendo cha Palestina kupewa hadhi ya mwanachama mwangalizi wa Umoja wa Mataifa asiye dola ndio uvunjaji mkubwa wa makubaliano ya amani ambao ulisimamiwa na chombo hicho cha kimataifa.
Afisa huyo anasema na hapa tunamnukuu " Watu wasishangae kuona Israel nayo inachukua hatua kujibu kitendo cha Wapalestina kusonga mbele na mipango yake kwenye Umoja wa Mataifa. Israel itachukua hatua zaidi kama Palestina nayo itaendelea na maamuzi yake binafsi ya kusonga mbele." mwisho wa nukuu.
Hapo jana Ufaransa, Uingereza na Sweden zilikosoa uamuzi wa Isreal wa kujenga makaazi 3000 wa walowezi kwenye Ukingo wa magharibi. Rais Francois Hollande wa Ufaransa alisema kuwa uamuzi huo unawapa wasiwasi.
Mataifa yanazidi kupaza sauti kuhusu hatua ya Israel ambapo sasa Uhispania, Italia, Norway na Uholanzi zimeitaka nchi hiyo kufikiria mara mbili mpango wake huo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Espen Barth Eide ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu ujenzi huo. Marekani ambayo ni mshirika mkubwa Israel imesema kuwa kitendo hicho ni kinyume na sera zake na kuitaka kuonyesha uvumilivu.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anatarajia kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Berlin kesho na watazungumza kuhusiana na suala hilo ambalo Ujerumani imesema linashusha uaminifu wa mataifa kwa Waisrael kuhusu kupatikana kwa amani baina yao na Wapalestina.
Palestina yenyewe imelaani hatua hiyo na kutaka jumuiya ya kimataifa kuichukulia hatua kali Israel na kusitisha ujenzi huo mara moja.
Mjumbe wa Palestina kwenye umoja wa matifa Riyad Mansour amesema kwenye barua alizoziiandika kwa Baraza la Usalama la umoja huo, Katibu Mkuu Ban Ki Moon pamoja na Hadhara Kuu ya umoja wa mataifa kwamba wakati viongozi wa taifa lake wakionyesha utayari wao wa mpango wa amani, Israel ndio kwanza inaendelea na vitenndo vyake vya uchokozi vilivyo kinyume na sheria.
Mwandishi: Stumai George/DPA/APE/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba