1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israeli na Lebanon wanajiandaa kwa vita visivyoepukika?

1 Februari 2024

Matarajio ya vita kamili kati ya Israel na wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon yanawatia hofu watu wa pande zote mbili za mpaka, lakini wengine wanauona kama mzozo usioepukika kutokana na vita vya Israel na Hamas.

Israel | Jeshi la Israel likifatua makombora kuelekea Lebanon
Jeshi la Israel likifyatua kombora kutoka kaskazini mwa Israel kuelekea LebanonPicha: Leo Correa/AP Photo/picture alliance

Vita kama hivyo vinaweza kusababisha madhara makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa na upande wowote. 

Israel na Hezbollah zina funzo kutokana na vita vyao vya mwisho, vilivyotokea mwaka 2006, vilivyodumu kwa mwezi mzima na kumalizika kwa kile wadadisi wa mambo walichokiita sare.

Pia wamekuwa na miezi minne ya kujiandaa kwa vita vingine, licha ya juhudi za Marekani kuzuia kuenea kwa mzozo kati ya Israel na Hamas. 

Vita vya 2006, miaka sita baada ya majeshi ya Israel kuondoka kusini mwa Lebanon, vilizuka baada ya Hezbollah kuwakamata wanajeshi wawili wa Israelna kuwaua wengine kadhaa katika shambulio la kuvuka mpaka.

Soma pia:Marekani yadai wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran walishambulia jeshi lake Jordan

Israel ilianzisha mashambulizi ya anga na ardhini na kuweka kizuizi ambacho kililenga kuwakomboa mateka na kuharibu uwezo wa kijeshi wa Hezbollah, katika oparesheni ambayo hatimaye ilishindwa.

Mwanamume akiwa amesimama katika kifusi baada ya jengo la makaazi kubomolewa kwa mashambulizi ya vikosi vya Israel, LebanonPicha: AFP

Mashambulizi ya Israelyalisawazisha maeneo makubwa ya Lebanon kusini na vitongoji vya kusini mwa Beirut, huku Hezbollah ikirusha maelfu ya maroketi yasioongozwa kuelekea jamii za kaskazini mwa Israeli.

Mzozo huo uliua Walebanon 1,200, wengi wao wakiwa raia, na Waisraeli 160, wengi wao wakiwa wanajeshi.

Azimio la UN likilenga kuleta utulivu

Azimio la Umoja wa Mataifa lililohitimisha vita hivyo lilitoa wito wa kuondolewa kwa vikosi vya Israel nchini Lebanon na kuundwa kwa eneo lisilo na shughuli za kijeshi kwenye upande wa mpaka wa Lebanon.

Licha ya kupelekwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, Hezbollah inaendelea kuendesha shughuli zake katika eneo la mpakani, huku Lebanon ikisema Israel inakiuka mara kwa mara mamlaka ya angayake na inaendelea kukalia maeneo ya ardhi ya Lebanon.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alionya mwezi uliyopita kuwa vita kati ya Israel na Hezbollah vitakuwa janga kamili, katikati mwa msusuru wa diplomasia ya Marekani na Ulaya.

Soma pia:UN: Hali katika hospitali za Gaza ni mbaya mno

Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah hajatishia kuanzisha vita lakini alionya kuhusu mapambano yasio na kikomo, ikiwa Israel itafanya hivyo.

Hezbollah inasema haitakubali kusitishwa kwa mapigano kwenye mpaka wa Israel-Lebanon kabla ya usitishwaji huo kutokea Gaza na imepinga pendekezo la Marekani la kuhamisha vikosi vyake kilomita kadhaa nyuma kutoka mpakani, kulingana na maafisa wa Lebanon.

Mwanamume akiwa amesimama katika kifusi baada ya jengo la makaazi kubomolewa kwa mashambulizi ya vikosi vya Israel, LebanonPicha: AFP

Licha ya matamshi makali kutoka pande zote, hakuna upande unaoonekana kutaka vita, anasema Andrea Teneti, msemaji wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon, na kuongeza hata hivyo kwamba makosa ya kihesabu yanaweza kusababisha mzozo mpana ambao ungekuwa mgumu kudhibitiwa.

Hezbollahna jeshi la Israeli wamepanua uwezo tangu 2006, lakini nchi zote mbili pia ni dhaifu zaidi, anasema Teneti.

Matokeo ya mgogoro na ustawi wa nchi

Nchini Lebanon, miaka minne ya mgogoro wa kiuchumi imedhoofisha taasisi za umma, ikiwa ni pamoja na jeshi lake na gridi ya umeme, na kuharibu mfumo wake wa afya.

Nchi hiyo inayohifadhi zaidi ya wakimbizi milioni 1 wa Syria, ilipitisha mpango wa dharura wa hali ya vita mwishoni mwa Oktoba, ikikadiria Waleboni milioni 1 wataihama nchi yao katika muda wa siku 45.

Israel inahisi matatizo ya kiuchumi na kijamii kutokana na vita vya Gaza, ambavyo vinatarajiwa kugharimu zaidi ya dola bilioni 50, au takriban asilimia 10 ya shughuli za kiuchumi za kitaifa hadi mwisho wa 2024, kulingana na Benki ya Israel.

Soma pia:Mawaziri wa Umoja wa Ulaya waijadili hali ya Gaza

Gharama zinatazamiwa kupanda sana ikiwa kutakuwa na vita na Lebanon.

Vita kamili vinaweza kuenea na kuhusisha pande nyingi, yakiwemo makundi ya uwakala wa Irani nchini Syria, Iraqi na Yemeni, na yumkini kuiingiza hata Iran yenyewe.

Vinaweza pia kuivuta Marekani, mshirika wa karibu wa Israel, zaidi katika mzozo huo, ambayo tayari imetuma imetuma meli za ziada za kivita katika eneo hilo.

Tahadhari kuhusu mdororo wa kiuchumi Lebanon

01:03

This browser does not support the video element.