ISTANBUL: Merkel asema Ujerumani itaheshimu ahadi za Umoja wa Ulaya kwa Uturuki
6 Oktoba 2006Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel amesema Ujerumani itazingatia ahadi za Umoja wa Ulaya zilizotolewa kwa Uturuki, ingawa chama chake kina shaka juu ya uanachama wa Uturuki katika umoja huo.
Akizungumza kwenye mkutano na viongozi wa kibiashara wa Ujrumani na Uturuki mjini Istanbul hii leo, kansela Merkel amesema anaunga mkono Uturuki iwe mshirika wa Umoja wa Ulaya atakayekuwa na faida maalumu.
Katika mahojiano yake na runinga ya ARD ya Ujerumani, Bi Merkel alisisitiza kuwa mazungumzo kuhusu uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya yatachukua muda mrefu.
´Hatuwezi kuamua swala hilo leo na hatutachukua uamuzi huo hivi leo pia.´
Wakati huo huo Bi Merkel na mwenyeji wake waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, wamekutana na viongozi wa kiislamu na kikristo, akiwemo Bartholomayo I, kiongozi wa kanisa la Orthodox duniani lenye wafuasi takriban milioni 200, ili kuhimiza mdahalo kati ya dini mbalimbali.