"Itachukua muda kwa Italia kuondokana na sumu ya utawala wa Berlusconi"
12 Aprili 2006Kulingana na mhariri wa gazeti la “Darmstädter Echo” Italia itabaki chini ya kivuli cha mamlaka ya Berlusconi hata baada ya yeye kushindwa. Mwandishi huyu ameandika:
“Prodi ameahidi kuiunganisha Italia. Na kwa kweli nchi hiyo inahitaji kiongozi anayeleta maridhiano. Silvio Berlusconi aliitenganisha Italia katika miaka mitano iliyopita ya mamlaka yake. Yule aliyempinga aliitwa mkomunisti au mhaini wa nchi. Hali ya kisiasa ilitiwa sumu. Kwa hiyo itachukua muda mrefu kwa nchi hiyo nzuri kuondokana na sumu ya utawala wa Berlusconi.”
Gazeti la “Süddeutsche Zeitung” linastaajabia ushindi wa Prodi dhidi ya mamlaka ya vyombo vya habari ya Berlusconi. Mhariri wa gazeti ameandika:
“Sasa Prodi amefanikiwa kumsimamisha Silvio Berlusconi ambaye alitawala kwa kutumia vyombo vya habari. Kiongozi huyu wa zamani bila ya kubarika macho alitumia kampuni zake za habari katika kugombea uchaguzi huu, alitaka kila kamera ipige picha yake, na kila mikrofoni irekodi sauti yake. Lakini hayo yote hayafua dafu. Kwenye siku ya uchaguzi profesa Prodi ambaye kwa kawaida si mcheshi alikuwa na sifa nzuri kuliko Berlusconi. Kwa hivyo hata katika demokrasia ya vyombo vya habari, yaliyosemwa yanashinda juu ya yaliyoonyeshwa. Hii ni habari nzuri kutoka Italia.”
Lakini gazeti la “Lübecker Nachrichten” lina wasi wasi juu ya serikali ya mseto ya Romano Prodi ya mrengo wa shoto na katikati. Limeandika:
“Muungano wa vyama chini ya uongozi wa Prodi unaunganisha vyama 17 vya kila aina – ikiwa ni cha kikomunisti, chama cha Christian Democrats, wanaharakati wa mazingira au Waliberali. Inawezekana kwamba mwanasiasa akinifu kama Prodi ambaye ni bingwa anayeaminika na mwenye uzoefu mkubwa katika siasa za Ulaya ni kiongozi anayefaa kuunganisha vyama hivi vingi. Lakini lengo lao la pamoja, yaani kumfukuza Berlusconi madarakani halipo tena.” - hayo ni maoni ya “Lübecker Nachrichten”.
Na mwisho ni gazeti la “Wiesbadener Kurier” ambalo linaona kwamba tofauti ya kura chache katika ushindi wa Prodi inaweza kuleta shida katika kuongoza Tunasoma:
“Kama ni uchumi, nakisi katika bajeti, suala la ajira au mfumo wa kijamii – kila mahali waziri mkuu wa zamani Berlusconi hajamaliza kazi yake. Hata hivyo karibu nusu ya wapiga kura walimchagua tena. Lakini sasa inabidi muungano wa mrengo wa shoto na katikati utekeleze mageuzi yaliyoahidiwa na mrengo wa kulia. Haijulikani vipi serikali hii mpya inaweza kushinda kwa kupata kura chache tu kuliko Berlusconi. Ikiwa mwakilishi mmoja tu katika baraza la seneti hakubaliani na Prodi, serikali hiyo inaweza kuvunjika.”