Itali na Ufaransa zaumaliza mvutano
14 Juni 2018Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameamua kuutatua mvutano na Itali akisema hakunuia kabisa kuichukiza nchi hiyo kwa hatua yake ya kukosoa kitendo cha kukataliwa meli ya wahamiaji ambayo ilisababisha ghadhabu mjini Rome. Jumanne Macron alisababisha mvutano mkubwa wa kidiplomasia ambao haujapata kuonekana katika kipindi cha miaka kadhaa kati ya Ufaransa na Itali kwa kuituhumu serikali ya mjini Rome kwamba ina ubinafsi na isiyowajibika kwa hatua yake ya kukataa kuwapokea wahamiaji 629 walioachwa wakihangaika katika meli ya uokozi ambayo hatimae ilipokelewa na Uhispania.
Itali ilimuita balozi wa Ufaransa kutaka ufafanuzi na ikaamua kufuta mkutano wa mawaziri uliopangwa kati ya nchi hiyo na Ufaransa kuhusu uchumi huku pia ikitoa kitisho cha kutaka kuufuta mkutano kati ya Macro na waziri mkuu Giusseppe Conte mjini Paris uliopangwa kufanyika Ijumaa. Itali imeitaka Ufaransa itoe tamko rasmi la kuomba radhi. Lakini mvutano huo unaonekana kupunguzwa makali baada ya Macro kumpigia siku usiku wa Jumatano waziri mkuu Conte.
Taarifa iliyotoka ofisi ya Macron imesisitiza kwamba matamshi yaliyotolewa na rais huyo hayakunuiwa kuikosea Itali na watu wake. Na Conte nae amewaambia waandishi habari mjini Rome kwamba mazungumzo yake na Macron yalikuwa mazuri sana na alipoulizwa ikiwa anahisi mvutano umemalizika alijibu kwa kusema ''Kwa kiasi kikubwa nafikiri ni hivyo,ndio umemalizika.''
Conte akasema kwamba sasa wanahitaji kushughulikia mageuzi ya makubaliano ya Dublin.
Makubaliano hayo yanasababisha mvutano mkubwa katika Umoja wa Ulaya kutokana na kipengele kinachosema kwamba wahamiaji wanahitajika kuomba hifadhi katika nchi ya kwanza wanayofikia. Sheria hioyo imeziweka katika shinikizo kubwa Itali na Ugiriki ambazo ni vituo vikubwa wanakofikia watu wanaokimbia vita na umasikini katika eneo la Mashariki ya Kati,Afrika na Asia.
Kabla ya tangazo la Conte la kuthibitisha atakwenda Paris Ijumaa,waziri mkuu Luigi Di Maio alisema Itali haitobadili msimamo wake kuelekea Ufaransa hadi pale nchi hiyo itakapoomba radhi na kusisitiza kwamba siku ambazo watu wanafikiri wanaweza kuinyooshea kidole Itali zimekwisha. Kisa cha meli ya uokozi ya Aquarius inayoelekea Uhispania kimeonesha kwa mara nyingine namna wanachama wa Umoja wa Ulaya walivyoshindwa kuwa na mshikamano linapohusika suala la wimbi la wahamiaji kupitia bahari ya Meditterania tangu mwaka 2015.
Mpango wa Umoja wa Ulaya wa kugawana wakimbizi sawa kwa sawa umeshindwa ambapo wanachama wa nchi za Ulaya ya Kati wamekataa katakata kukubaliana na suala la kuchukua kiwango cha wakimbizi wakati nchi nyingine ikiwemo Ufaransa ikishindwa kuchukua kiwango chote cha wakimbizi ilichowekewa. Mashirika ya hisani yametahadharisha kuhusu kiwango cha mgogoro huo unavyogharimu maisha ya wahamiaji. Alhamisi watu wanne walihukumiwa kifungo cha miaka 25 jela nchini Hungary kuhusiana na mauaji ya kutisha ya wahamiaji 71 waliofungiwa ndani ya lori hadi kufa katika barabara kuu ya kwenda Austria miaka mitatu iliyopita.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman