1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia waandamana kuwaunga mkono Wapalestina

23 Septemba 2025

Maandamano makubwa yamefanyika nchini Italia kupinga vita vya Israel ambapo waandamanaji walitaka kusitishwa kwa mauaji, katika wakati huu jeshi la Israel likiendelea na operesheni ya ardhini kwenye Jiji la Gaza.

Italia Milan 2025 | maandamano ya Gaza
Maandamano ya raia wa Italia dhidi ya mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza yaliyofanyika siku ya Jumatatu (Septemba 22, 2025) katika mji wa Milan.Picha: Alessandro Bremec/IPA/ZUMA/picture alliance

Umati wa waandamanaji nchini Italia walimiminika mitaani siku ya Jumatatu (Septemba 22), wakipaza sauti zao dhidi ya mauaji yanayoendelea kwenye Ukanda wa Gaza.

Maandamano hayo ya aina yake yaliyoitishwa na vyama vya wafanyakazi, yaliwajumuisha walimu na wanafunzi wa vyuo vikuu, wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi, madereva wa mabasi na matreni na wafanyakazi wa bandari.

Wakionesha hasira zao mbele ya vurugu za polisi, waandamanaji hao walitaka  mashambulizi dhidi ya Gaza  yakomeshwe mara moja na kuitolea wito serikali ya mrengo mkali wa kulia kuiwekea vikwazo Israel mara moja.

Wengine walielezea kuwa hatimaye mauaji yanayofanyika Gaza yamewafumbua macho na kuujuwa ukweli ambao walidai kuwa siku zote "ulikuwa umefichwa."

"Umati kama huu haujawahi kuonekana kwa muda mrefu. Tena kukusanyika kwa kuonesha mshikamano na wenzetu na sio kudai maslahi ya kiuchumi. Palestina inawakilisha sio tu alama ya mapambano ya muda mrefu bali pia kuporomoka kwa uongo uliojengwa siku nyingi dhidi yake. Tulikuwa tunaambiwa mambo mabaya tu kuhusu Wapalestina. Sasa ni wakati ambapo kila kitu kipo wazi."  Alisema Sabina Guzannti, mmoja wa waandamanaji hao.

Waandamanaji wakikabiliana na polisi wa kutuliza fujo kwenye maandamano ya kupinga mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza yaliyofanyika Milan, Italia, siku ya Jumatatu (Septemba 22, 2025).Picha: Francesco Enriquez/IPA/ZUMA/picture alliance

Mbali ya mji maarufu wa Milan, maandamano hayo yaliyosindikizwa na mgomo wa masaa 24 yalishuhudiwa pia katika mji mkuu wa Italia, Rome, na katika bandari mbili kubwa za Genoa na Livorno. 

Mashambulizi yaendelea Gaza

Siku ya Jumanne (Septemba 23) Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina lilichapisha mkanda wa video unaoonesha wafanyakazi wa huduma ya afya wakikusanya miili sita ya Wapalestina waliouawa katika Jiji la Gaza.

Miili hiyo iliyopatikana kwenye njiapanda ya Maliya katika kiunga cha Tal al-Hawa ilipelekwa baadaye kwenye Hospitali ya Shifa, mojawapo ya majengo machache yaliyosalia kufanya kazi licha ya nalo kushambuliwa mara kwa mara na jeshi la Israel. 

Hali ilivyo kwenye Ukanda wa Gaza unaokabiliwa na mashambulizi ya kila mara ya jeshi la Israel. Picha: Ammar Awad/REUTERS

Idadi ya Wapalestina waliokwishakuuawa tangu  Israel ianze vita vyake kwenye Ukanda wa Gaza baada ya uvamizi wa wanamgambo wa Kipalestina kusini mwa Israel mnamo Oktoba 2023, imefikia 65,344, huku wengine 166,795 wakiwa wamejeruhiwa. 

Hisabu hii iliyotolewa siku ya Jumanne na mamlaka za afya kwenye Ukanda huo inajumuisha tu wale ambao wametambuliwa rasmi, ingawa wafuatiliaji wa mambo wanasema idadi kamili ni kubwa zaidi ya hapo, huku wataalamu wa Umoja wa Mataifa wakiyatambuwa mauaji hayo kufikia kiwango cha "maangamizi ya kimbari."

Ndani ya kipindi cha masaa 24 tu yaliyopita, mashambulizi ya Israel yalikkuwa yamewauwa watu 61 na kuwajeruhi wengine 220 kwenye Jiji la Gaza pekee, kwa mujibu wa taarifa hiyo. 

Hospitali mbili ndani ya Jiji hilo zililazimika kusitisha huduma zake wakati operesheni ya ardhini ya jeshi la Israel ikiendelea kaskazini mwa Gaza.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW