1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia yaanza kuimarisha doria baharini

14 Oktoba 2013

Italia imesema itaimarisha doria kusini mwa bahari ya Mediterania, katika juhudi za kuzuia kutokea tena kwa maafa kama yale ya hivi karibuni, ambapo mamia ya wahamiaji kutoka Afrika walikufa katika ajali mbaya za boti.

Italia inanuia kuwa na uwezo zaidi wa kuzing'amua meli za wahamiaji katika bahari ya Mediterania
Italia inanuia kuwa na uwezo zaidi wa kuzing'amua meli za wahamiaji katika bahari ya MediteraniaPicha: Getty Images

Waziri Mkuu wa Italia, Enrico Letta, amesema juhudi hizo mpya zitaanza leo Jumatatu kusini mwa kisiwa cha Sicily, ambako boti chakavu zimekuwa zikipita, zikibeba maelfu ya wahamiaji wanaotoka Afrika.

Ijumaa iliyopita, wahamiaji 34 walikufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama. Hata hivyo kwa mujibu wa wanamaji wa Italia, idadi ya walioangamia katika ajali hiyo ni kubwa zaidi ikizingatiwa kuwa maiti nyingi bado hazijapatikana.

Ajali mbili chini ya wiki mbili

Ajali hiyo ya wiki iliyopita ilifuatia nyingine ya tarehe 3 Oktoba ambapo watu zaidi ya 350 walipoteza maisha. Walionusurika ajali ya wiki iliyopita walisema boti yao ilifyatuliwa risasi na watu wanaoshukiwa kuwa Walibya, ingawa hawakuweza kuwatambua kikamilifu kwa sababu walikuwa mbali.

Wahamiaji wengi kutoka Afrika wameangamia baharini mnamo wiki 2 zilizopitaPicha: picture-alliance/dpa

Waziri Mkuu wa Libya Ali Zeidan amekanusha kuhusika kwa jeshi la nchi yake, na kuahidi kuyafanyia uchunguzi madai hayo.

Wengi wa wahamiaji hupanda boti kwenye pwani ya Libya, lakini serikali ya Italia ina wasiwasi kuwa idadi ya wahamiaji inayozidi kupanda inatoka katika nchi zenye misukosuko kama Syria na Misri.

Waziri wa ulinzi wa Italia, Mario Mauro, ameliambia gazeti la Avvenire linalochapishwa kila siku nchini humo, kuwa doria katika bahari ya Mediterania itaongezwa mara 3, katika operesheni ya kijeshi na ya kibinaadamu, kutokana na ukweli kwamba kwa sasa Libya inachukuliwa kama nchi isiyo na utawala wa kitaifa.

"Inatubidi kuchukua hatua kali kuzuia boti hizo chakavu kuingia baharini", amesema Mauro na kuongeza kuwa mipango ya kifedha na kimkakati inakamilishwa ili kutuma meli na vifaa vyenye uwezo bora zaidi kuzing'amua boti hizo.

Ndege isiyo na rubani kutumiwa

Vyombo vya habari vya Italia vimesema kuwa ndege isiyokuwa na rubani yenye kituo katika kisiwa cha Sicily, inaweza kutumiwa kuzitambua boti ambazo ziko hatarini.

Pamoja na walinzi wa pwani na polisi wa kulinda mpaka, jeshi la baharini la Italia hufanya doria kutumia meli tatu na helikopta nne, pamoja na ndege mbili zenye vifaa vya kusaidia kuona wakati wa giza.

Rais wa halmashauri kuu ya Ulaya Jose Manuel Barroso na waziri mkuu wa Italia Enrico Letta wakizungumzia suala la wahamiajiPicha: picture-alliance/dpa

Maafisa wa jeshi la kulinda pwani ya Italia wamesema kwamba jana Jumapili meli zao ziliwaokowa wahamiaji 400 ambao boti yao ilikuwa ikikabiliwa na hatari ya kuzama, na boti nyingine iliyowabeba wahamiaji 100 iliokolewa na wanamaji wa kisiwa cha Malta.

Mamlaka ya kisiwa hicho jana yaliutolea wito Umoja wa Ulaya kuweka sera inayoeleweka kushughulikia wahamiaji wanaomiminika kwenye ufukwe wa kisiwa hicho, wakikimbia machafuko katika nchi zao.

Waziri Mkuu wa Malta Joseph Muscat alisema ingawa wao sio taifa kubwa, majukumu yanayowakabili sio tu kulinda mipaka yao, bali pia mipaka ya Umoja wa Ulaya, kama vile inavyofanya Italia.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/RTRE

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi