1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia yaipa Libya jukumu la uokozi wa wahamiaji

6 Julai 2018

Italia imekabidhi jukumu la shughuli za uokozi wahamiaji wanaovuuka Bahari ya Mediterenia kuwania kuingia Ulaya kwa taifa la Libya ikiwa ni moja ya hatua ya kuwazuwia wahamiaji hao.

Libyen Migranten auf Marine-Boot
Picha: Reuters/I. Zitouny

Katika mkutano wa Umoja wa Ulaya wiki moja iliyopita, viongozi wa Ulaya kwa mara nyengine tena walikubaliana kulinda mipaka ya nje ya nchi zao dhidi ya wahamiaji wanaojaribu kuingia barani humu kinyume cha sheria, hiyo ikimaanisha kupinga uhamiaji kupitia Bahari ya Mediterenia kati ya Italia na Libya.

Aidha serikali mpya ya Italia, imeshaanza kuchukua hatua zaidi. Mwishoni mwa mwezi Juni, ilizuwiya boti moja  kuingia bandari ya Italia, ilikokuwa inawaleta waomba hifadhi waliookolewa. Baadaye ikakubaliana na Libya kuwa inaipa tena jukumu la kuwaokoa wahamiaji wanaoingia nchini humo.

Jeshi la majini la ItaliaPicha: Imago/Xinhua

Italia awali ilibeba jukumu la uokozi katika eneo zima la bahari kati ya eneo lake na Libya, huku jeshi la majini la Italia likiratibu shughuli zote za kuwatafuta na kuwaokoa wahamiaji.

Hata hivyo, hatua hiyo ya kuipa tena Libya jukumu la uokozi wa wahamiaji imezidi kukosolewa na baadhi ya mashirika ya  usafiri wa majini, Michael Buschheuer, muanzilishi wa shirika binafsi la Sea-Eye, ameiambia DW kwamba haelewi na haoni sababu kwa nini Libya ndiyo iliyopewa jukumu la shughuli za uokozi miongoni mwa nchi zote zilizopo.

Buschheuer, alikuwa akitolea mfano ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa iliyoripoti juu ya madhila ya wahamiaji wanaorejeshwa nchini Libya, kwamba baadhi yao wanapitia mateso na hata kubakwa, wanakandamizwa na saa nyengine wanatupwa jangwani.

"Libya ni nchi ambayo haipaswi kuchukua jukumu la shughuli ya uokozi wa wahamiaji, lakini hiyo ndio hali halisi iliyopo kwa sasa," alisema Buschheuer.

Waangalizi wengine wanasema kwamba wanashuku Italia ina matumaini kwamba walinzi wa fukwe za bahari wa Libya watazirejesha meli binafsi, huku wakisema kuwa Umoja wa Ulaya unakiuka sheria ya kimataifa kwa kuridhia waomba hifadhi kurejeshwa nchini Libya.

wakimbizi na wahamiaji katika bahari ya Mediterenia akionekana kuomba msaada baada ya boti yao kuzama majiniPicha: Getty Images/C. McGrath

Lakini hali ilivyo kwa sasa imebadilika, tarehe 22 mwezi Juni Libya ililijulisha shirika la kimataifa la usafiri wa Baharini la Umoja wa Mataifa IMO kwamba iko tayari kuridhia matakwa yote yanayohitajika juu ya shughuli za uokozi. Tayari taifa hilo limepokea boti 12 kutoka Italia na Umoja wa Ulaya umewekeza fedha nyingi kutoa mafunzo kwa walinzi wa pwani wa Libya.

Kutokana na Libya na Malta kuzuwiya baoti binafsi zilizobeba wahamiaji kuingia nchini humo idadi ya wahamiaji wanaozama majini inazidi kupanda,  hii ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la IOM. Msemaji wa shirika hilo, Flavio di Giacomo, ametoa wito wa mataifa zaidi kutuma meli za uokozi ilikuzuwiya vifo vya wahamiaji zaidi.

Mwandishi: Amina Abubakar/DW Page

Mhariri: Mohammed Khelef