Italia yakabwa na Berlusconi
30 Septemba 2013Tunaanzia Italia ambako mgogoro wa kisiasa umezidi makali baada ya mawaziri watano wa kutoka chama cha Silvio Berlusconi kujiuzulu.Gazeti la "Saarbrücker Zeitung" linaandika:
Italia iko hatarini.Kila siku inapopita bila ya serikali kuwa na uwezo wa kuwajibika ndipo nayo hatai inapozidi kuongezeka: Mzigo wa madeni yanayoikaba nchi hiyo unakua,vitega uchumi vinapungua,shughuli za kiuchumi zinazorota na idadi ya wasiokuwa na ajira inaongozeka.Mzozo unapozuka Roma na kitisho cha kupooza shughuli za kiuchumi kinaongezeka.Berlusconi anacheza na mustakbal wa wakaazi wa nchi hiyo.Mbinu zake za kisiasa hatimae zitawadhuru wananchi.
Berslusconi acheza na hatima ya Italia
Maoni sawa na hayo yametolewa pia na gazeti la "Westfälische Nachrichten" linalohisi:"Mtu huyo aliyehukumiwa kwa makosa ya kugushi malipo ya kodi ya mapato anaiteka nyara nchi nzima.Berlusconi,kutokana na sababu za kibinafsi anaicha ivunjike serikali ya nchi hiyo inayozongwa na mizozo.Kwa wakati wote ambao Berlusconi atatoka katika kifungo cha nyumbani na kutaka kutawala, naiwe,binafsi au kupitia vyombo vyake vya habari,basi na Italia nayo haitatoka katika hali ya mtafaruku."
Mazungumzo ya kuunda serikali Ujerumani
Kishindo kinakutikana pia nchini Ujerumani baada ya uchaguzi mkuu wa September 22 iliyopita.Nani atashirikiana na nani kuunda serikali?Kwa mujibu wa vyombo vya habari Duru ya mwanzo ya kupima maoni itafanyika ijumaa ijayo kati ya vyama ndugu vya Christian Democratic Union,CDU na Christian Social Union CSU vilivyojikingia wingi wa kura,na Social Democratic SPD.Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linaandika:Juhudi zimeshika kasi,vyama vinvyowakilishwa katika bunge la shirikisho Bundestag vinaanza kugutuka.Wasocial Democrats wanaojiamini kupita kiasi hawana budi isipokua kuzungumza na wana CDU na CSU hata kama mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano hayakuwa rahisi.Vizingiti viko vingi na vinawekwa na kila upande.Na hasa na mwenyekiti wa chama cha Christian Social Union-CSU, Horst Seehofer anaesema hatotia saini mkataba wa kuunda serikali ya muungano kama suala la kulipishwa kodi madareva wa nchi za nje halitaingizwa.Na sasa anazidisha makali kwa kusema hatosaini pia kama mkataba huo utazungumzia kuhusu kupandishwa kiwango cha kodi ya mapato.
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu mzozo uliosababishwa na mradi wa kinuklea wa Iran.Katika wakati ambapo rais mpya wa iran Hassan Ruhani anajaribu kuwajongelea walimwengu,kuna wanaoshuku kama dhamir zake ni za dhati.Gazeti la "Fränkischer Tag" linahisi njia moja tu ndio itakayoweza kusaidia:Gazeti linaendelea kuanadika:"Uwazi ndio njia pekee itakayorejesha imani ya walimwengu katika mvutano uliosababishwa na mradi wa kinuklea.Na ahadi zitabidi zifuatiwe na vitendo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman