Italia yatangaza hatua kali kupambana na Corona
8 Machi 2020Hatua hiyo imesababisha kuparaganyika kwa mipango ya safari baada ya kuwekwa zuio kwa takribani robo ya idadi ya raia nchini humo kusafiri, kutoka sehemu moja kwenda nyingine ikiwa ni katika juhudi za kupambana na kuendelea kusambaa kwa maambukizi ya virusi hivyo.
Waziri mkuu wa Italia mapema leo, Giuseppe Conte alitia sahihi sheria itakayowaathiri takribani watu milioni 16 katika eneo tajiri la kaskazini mwa nchi hiyo, ukiwemo mkoa wa Lombardy na mikoa 4 jirani. Hatua hiyo kali itadumu hadi Aprili 3.
Conte amenukuliwa akisema "Kwa Lombardy na mikoa mingine ya Kaskazini ambayo nimeiorodhesha, kutakuwa na marufuku ya watu kuingia na kutoka kwenye maeneo hayo." Waziri mkuu huyo wa Italia amesema ruhusa pekee za kutoka na kuingia kwenye maeneo hayo zitatolewa kwa mahitaji ya kitaalamu yaliyothibitishwa, visa vya kipekee na masuala ya kiafya.
Duniani kote, nchi nyingine zimekuwa zikiiga mfano wa China ambapo ndiko chimbuko la Virusi hivyo kwa kuweka udhibiti wa safari na kufuta hafla za umma. Hadi sasa China ina visa 106,000 na takribani vifo 3,600 vinavyotokana na maambukizi ya virusi vya Corona.
Mtafaruku saa chache kabla ya tamko la Conte
Saa kadhaa kabla ya Waziri Mkuu Conte kutia saini sheria ya kudhibiti eneo lililoathirika na virusi vya Corona, taifa hilo lilikumbwa na mtafaruku baada ya kuvuja kwa taarifa juu ya mpango wa kuyaweka Karantini maeneo husika.
Wanafunzi katika Chuo kikuu cha Padua Kaskazini mwa Italia ambao walikuwa matembezini Jumamosi usiku walipata tetesi hizo kupitia simu za mkononi na kurejea haraka kwenye makazi yao kuchukua vitu vyao na kuelekea katika kituo cha treni. Mamia ya abiria wengi walionekana wakiwa wamejifunika kwa barakoa na kuvaa glavu mikononi mwao
Hatua kali za kuiweka karantini mikoa ya Kaskazini mwa Italia zimechukuliwa baada ya Italia kutangaza hapo jana ongezeko kubwa la maambukizi ya virusi vya Corona kwa siku moja tangu kuanza kusambaa kwa virusi hivyo, Februari 21. Idadi ya watu walioathiriwa ilikuwa watu 1,247 katika saa 24 zilizopita na kufikia 5,883. Idadi ya vifo nchini humo hadi sasa imefika 233.