1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia yatangaza maombolezo Kitaifa

26 Agosti 2016

Italia imetangaza maombolezo ya kitaifa kufuatia vifo vya watu 267 raia wa nchi hiyo na wageni waliopotea maisha katika tetemeko la ardhi linalokisiwa kuwa na ukubwa wa 6.2 lililotokea mapema siku ya Jumatano wiki hii.

Muokoaji akitembea katika moja ya nyumba zilizoharibiwa na tetemeko hiloPicha: Getty Images/AFP/M. Zeppetella

Maombolezo hayo ya kitaifa yatafanyika Jumamosi hii karibu na mji wa Ascoli Piceno, wakati bendera ya nchi hiyo itapeperushwa nusu mlingoti.

Kwa upande mwingine, zoezi la uokoaji linaendelea katika baadhi ya meneo ili kupata miili ya watu au waliojeruhiwa na kunasa katika vifusi huku watu wengine zaidi ya watu 2,500 wakiwa wameachwa bila makaazi.

Moja kati ya maeneo ambayo uokoaji unaendelea ni katika mji wa kitalii wa Amatrice mji ambao umeathiriwa sana na tetemeko hilo ambako kwa sasa ni nadra sana kuona jengo katika mji huo wa zamani ambao umewahi kujulikana kama mji wenye vyakula vizuri zaidi vya asili ya Italia. Mpaka sasa wamefakiwa kupata miili ya watu 207.

Msichana wa miaka 10 ambaye aliokolewa kutoka katika kifusiPicha: picture-alliance/AP/Sky Italia

Kitengo cha ulinzi wa raia mjini Rome kinasema karibu watu 400 wanapatiwa matibabu ya majeraha katika hospitali mbalimbali na 40 kati yao wako katika hali mbaya zaidi huku wakiongeza kuwa manusura ambao hawana sehemu ya kwenda wametengenezewa sehemu maalumu ambako kuna mahema na huduma za dharura.

Akisimulia namna walivyokumbwa na zilzala hiyo, Anna Maria, mmoja kati ya walionusurika, anasema "ulikuwa ni usiku wa aina yake kwa sababu kulikuwa na mabadiliko makubwa ya hali ya hewa, kulikuwa na joto kali sana wakati wa mchana na kulikuwa na baridi kali sana pia wakati wa usiku."

Serikali yaahidi kusaidia wahanga

Waziri Mkuu Matteo Renzi ametangaza hali ya dharura na kuruhusu serikali kutoa pesa kiasi cha euro milioni 50 kwa ajili ya kusaidia zoezi la uokoaji na pia ameahidi kusimamia zoezi la kuzijenga upya nyumba zilizoharibiwa na tetemeko hilo huku.

Ripoti zinasema kuwa Italia inarekodi mbaya ya kujijenga upya baada ya kutokea kwa matetemeko ambapo mpaka sasa kuna watu 8,300 walilazimika kuyahama makazi yao baada ya kutokea kwa tetemeko katika mji wa L'Aquila mwaka 2009 ambao mpaka sasa wanaishi katika nyumba ambazo si za kudumu.

Majengo mengi yalijengwa miaka ya zamani iliyopita yameharibiwa vibaya, ikiwa inajumuisha maeneo 293 ya kihistoria mengi yakiwa ni makanisa ambayo yamebomolewa kiasi na mengine kuharibiwa kabisa.

Karibu watu 30 walipoteza maisha katika tetemeko lililowahi kutokea kaskazini mwa nchi hiyo mwaka 2012 na wengine zaidi ya 300 walipoteza maisha kwenye tetemeko lililotokea L'Aquila

Mwandishi: Celina Mwakabwale/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef