Ivory Coast yapata ushindi wa dhidi ya Guinea ya Ikweta
13 Januari 2022Gradel, akiwa nahodha wa kikosi thabiti cha Ivory Coast ambacho kilikuwa na winga wa Crystal Palace akiwa kwenye benchi la akiba, alifunga bao kali katika dakika ya sita wakati walianza mechi kwa kasi ya ajabu katika dimba la Japoma mjini Douala.
Lakini wakati Ibrahim Sangare alikuwa na nafasi mbili za kuongeza mabao kabla ya kipindi cha mapumziko, Guinea ya Ikweta, moja ya nchi ndogo kabisa za Afrika, ilidhihirisha kuwa timu ngumu kuifunga. Vibonde hao walikuwa na nafasi kadhaa nzuri wakati walicheza kandanda bila kuwaogopa wapinzani wao ambao ni miamba ya Afrika.
Timu hizo mbili ndio zilikuwa za mwisho kushuka dimbani katika mashindano hayo huku timu zote 24 zinazoshiriki sasa zikiwa zimecheza mechi moja kila mmoja. Yalikuwa ni matokeo ya ushindi wa 1-0 katika mechi tisa kati ya 12 za ufunguzi.
Ivory Coast wanaongoza kundi hilo baada ya mabingwa watetezi Algeria kukabwa kwa sare tasa na Sierra Leone mjini Douala jana.
Katika Kundi F, Gambia ambayo inashiriki mashindano hayo kwa mara yao wa kwanza waliwapiga Mauritania 1-0 katika mechi iliyopigwa mjini Limbe na kugubikwa na utata uliozunguka mechi ya mapema ambayo Mali ilishinda kwa matokeo saw ana hayo dhidi ya Tunisia.
Bao pekee la Gambia lilifungwa na Abilie Jallow. Wakiwa chini ya kocha mwenye uzoefu Mbelgiji Tom Saintfiet, Gambia wanashiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza baada ya majaribio 16 yaliyoshindwa kufuzu.
Mechi hiyo ilicheleweshwa kwa dakika 45 kwa sababu mwamuzi wa mechi ya kwanza alikosea kwa kumaliza mechi hiyo dakika tatu kabla ya dakika 90. Refarii Mzambia Janny Sikazwe alipuliza kipyenga cha kumaliza mechi baada ya dakika 89 na sekunde 47 wakati mechi ilipaswa kumalizika dakika 93, ukiwemo muda wa nyongeza.
Kufuatia malalamiko kutoka kwa Watunisia waliojawa hasira, akiwemo kocha Mondher Kabaier, wasimamizi wa mechi waliondoka uwanjani wakisindikizwa na maafisa wa usalama.
Wakati wa vikao vya waandishi wa Habari, timu hizo ziliarifiwa kuwa mechi lazima iendelee kwa sababu ilikuwa imemalizika kabla ya muda rasmi.
Mali ilitii, lakini Tunisia ikakataa kwa sababu tayari wachezaji walikuwa wakipoza misuli kwenye barafu, kwa mujibu wa kocha Kebaier.
Kukataa kwa Tunisia kurejea uwanjani huenda kukawaweka katika hatari ya kuadhibiwa na waandalizi wa mashindano hayo, Shirikisho la Kandanda Afrika - CAF.
Mali ilipata ushindi kupitia penalti kunako dakika ya 48 ikifungwa na Ibrahima Kone wakati nahodha wa Tunisia Wahbi Khazri akishindwa kufunga penalti. Mechi inayofuata ya Gambia ni dhidi ya Mali uwanjani Limbe Jumapili, kisha itafuatiwa na Mauritania dhidi ya Tunisia katika dimba hilo
Hii leo wenyeji Cameroon watashuka uwanjani kupambana na Ethiopia wakati Cape Verde ikiwa na kibarua dhidi ya Burkina Faso katika mechi za Kundi A
afp