Jackson afurahi kujiunga na miamba Bayern Munich
15 Septemba 2025
Mshambuliaji mpya wa Bayern Munich, Nicolas Jackson, amesema leo Ijumaa 12.09.2025 kwamba amefurahi kuwa "mahali anapohitajika" baada ya kujiunga na miamba hao wa Ujerumani kwa mkopo wa msimu mzima akitokea klabu ya Ligi Kuu ya Premia, Chelsea.
Wakati wa kutambulishwa kwake rasmi mjini Munich, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 amezungumzia kuhusu "changamoto na hali ngumu" zilizomkumba baada ya mkataba wake wa mkopo kukaribia kuvunjika siku chache kabla ya dirisha la uhamisho kufungwa.
"Katika kandanda, kunatokea wakati ambapo mchezaji anahitaji mabadiliko. Nilizungumza na mkurugenzi wa michezo wa Bayern Munich Max Eberl pamoja na kocha na walitaka sana niwe hapa na walinipenda.” Ameongeza kuwa, "Kama mchezaji, unataka kuwa sehemu ambapo watu wanakuhitaji."
Jackson, ambaye alijiunga na Chelsea mwaka 2023, alipoteza nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza cha "The Blues" kufuatia usajili wa majira ya kiangazi wa Joao Pedro na Liam Delap.
Mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Senegal aliwasili mjini Munich kuelekea siku ya mwisho ya dirisha la uhamisho na kutia saini mkopo wa mwaka mzima japo baadaye alitakiwa kurejea Chelsea baada ya Delap kupata jeraha.
Kupitia wakala wake, Jackson alisisitiza kuwa hatorudi London akitaka kusalia Bayern.
Bayern Munich ilitangaza usajili wake saa chache baada ya dirisha kufungwa, wakikubaliana ada ya mkopo ya milioni €16.5 na wajibu wa kumnunua kwa milioni €65. Hata hivyo, kiongozi wa klabu Uli Hoeness alisema masharti hayo yamewekewa vigezo vigumu kutimizwa, ikiwemo Jackson kuanza mechi 40 msimu huu.
"Tunapaswa kulipa fedha hizo iwapo Jackson ataanza mechi 40 msimu huu. Hilo halitawahi kutokea," Hoeness alisema siku ya Jumanne.
Jackson amemtaja Hoeness kuwa "gwiji wa klabu" lakini akaongeza kwamba kutimiza wajibu wa kumnunua "sio uamuzi wangu, sio jambo linalonilenga. Jukumu langu ni kucheza uwanjani na kufunga magoli mengi kadri niwezavyo na kuisaidia timu kushinda."
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Villarreal anatarajiwa kucheza mechi yake ya kwanza akiwa na nyuzi nyekundu Jumamosi 13.09.2025 wakati Bayern watakapowakaribisha Hamburg uwanjani Allianz Arena.