Jacob Zuma asema hana hatia.
4 Januari 2008Johannesburg.
Kiongozi mpya wa chama tawala nchini Afrika kusini ANC, Jacob Zuma , ameahidi leo kuwa yuko tayari kupambana mahakamani kuthibitisha kuwa hana hatia ya madai ya rushwa yanayotolewa dhidi yake.
Jacob Zuma ameliambia gazeti la Afrikaaner Beeld katika mahojiano yake ya kwanza tangu kushtakiwa kwa madai ya rushwa wiki moja iliyopita.
Zuma ambaye amechaguliwa kuongoza chama tawala cha ANC wiki mbili zilizopita, alishtakiwa rasmi hapo Desemba 28 kwa madai ya rushwa, kughushi nyaraka, kutumia fedha zilizopatikana kwa njia haramu, ulaghai na ukwepaji kodi kufuatia uchunguzi ambao pia umelihusisha kampuni ya utengenezaji wa silaha la Ufaransa, Thales. Kesi ya Zuma inaanza August 14.
Washirika wake wamemtetea sana tangu pale aliposhtakiwa, wakidai kuwa ni mhanga wa kisasi cha kisiasa. Afisa mmoja wa chama cha wafanyakazi cha COSATU ameonya jana kuwa kunaweza kutokea ghasia iwapo Zuma atapatikana na hatia.