Jaji Chande: Hatukutegemea vyanzo vya polisi pekee
28 Aprili 2026
Mwenyekiti wa Tume ya kuchunguza vurugu za Oktoba 29 wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Jaji Mstaafu, Mohamed Othman Chande amezungumza na wanahabari leo na kutoa ufafanuzi wa ripoti hiyo.
Akizungumza na wanahabari Jaji Chande amefafanua hoja kadhaa zilizoibua maswali baada ya ripoti yake kuwasilishwa mbele ya rais na kusema ripoti hiyo haikuegemea ushahidi wa jeshi la polisi, bali ilikusanya taarifa kutoka katika jeshi hilo ikiwamo suala la kupotea kwa watu kama chanzo cha vurugu hizo.
Jaji Chande amesema, moja ya chanzo cha vurugu hizo ni kupotea kwa watu ambapo takwimu za jeshi la polisi zinaonyesha kuwa ya mwaka 2023 na 2025 watu 758 walipotea na kati yao 503 walipatikana.
Kadhalika Jaji Chande amefafanua hoja ya uwajibishwaji baada ya kuwepo kwa malalamiko kuwa waliohusika na kuchochea kwa vurugu hizo kwa namna moja au nyingine hawajawajibishwa. Jaji Chande amesema, tume ilitoa ramani ya uwajibikaji.
"Safu ya kwanza ni uwajibikaji binafsi wa mtu aliyeshiriki kutenda kosa la madai, kwa polisi, si jambo geni kwanza sheria inasema hivyo, kwamba askari polisi atakayesababaisha mauaji kwa kutumia silaha, atawajibika yeye mwenyewe binafsi.”
Wajumbe wa tume hiyo walielezea namna walivyokusanya ushahidi wa kisayansi na kwa kutumia mahojiano ikiwamo kufanya uchunguzi wa sababu ya vifo hivyo na kupata idadi kamili.
Awali makundi ya wanaharakati, wanasheria na vyama vya siasa wametoa kasoro za ripoti hiyo wakiinyoshea kidole kwa kutoweka wazi masuala muhimu ikiwamo idadi ya watu waliofariki, ukusanyaji wa ushahidi na uwajibishwaji wa wahusika.
Mjumbe wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Profesa Ibrahim Juma amesema.
"Sisi, kama Tume, baada ya kukaa na kusikiliza ushahidi wote, maoni yetu yanaweza kuwa tofauti na yale ya watu au vikundi ambavyo havikupata fursa ya kusikiliza mashahidi na kupitia nyaraka husika. Mapendekezo yetu yanatokana na ushahidi wa moja kwa moja tulioupata kupitia kukutana na watu, na siyo ya kinadharia”
Ripoti yapokelewa kwa mitazamo tofauti
Jaji Juma amesema mara baada ya tume hiyo kuwasilisha ripoti yake mbele ya rais, walipokea simu za matusi zaidi ya 300 zikiwashutumu kuhusu ripoti hiyo.
Jaji Chande amesema, tume hiyo haijakataa kuwawajibisha waliohusika na vurugu hizo na kueleza kuwa, wamependekeza kufanya uchunguzi maalum wa vifo visivyo vya kawaida ikiwamo vya watoto 21 .
Wajumbe wa tume hiyo wamesema, wamesikiliza mashahidi 40 kwa siku moja ana kwa ana, kwa barua, meseji za makundi sogozi na waliojaza madodoso ni jumla ya watu 62,700.
Tume hii iliundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Novemba 18 mwaka jana na imefanya kazi kwa siku 153 hadi ilipowasilisha ripoti yake kwa Rais, mnamo Aprili 23.