Jaji Mkuu Kenya ataka bunge livunjwe
22 Septemba 2020Katika hatua ambayo haikutarajiwa, Jaji Mkuu Maraga alisema siku ya Jumatatu (Septemba 22) kuwa Bunge limeshindwa kuzingatia uamuzi wa mahakama wa kuunda sheria ya kutekeleza sheria itakayoruhusu thuluthi mbili ya wabunge wa kike kwa kipindi cha miaka tisa sasa. Kanuni hiyo inalenga kusawazisha idadi ya wanawake bungeni ambako idadi kubwa ya wabunge ni wanaume.
Akitoa taarifa hiyo, Jaji Maraga alisema alitumia mamlaka ambayo katiba imempa kumshauri rais kulivunja bunge. Kisheria baada ya hapo, maspika wa mabunge mawili wanatakiwa kufahamisha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuhusu hatua hiyo.
Iwapo hilo litafanyika, wabunge wote watahitaji kuwania tena nafasi zao kwenye uchaguzi mdogo.
Wanasheria wanasema kuwa uongozi wa taifa umeshindwa kuzingatia na kutii sheria.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria, Nelson Havi, anasema kuwa wabunge kwa sasa wanavunja sheria kwa kuwa bungeni. "Rais anatakiwa kulivunja bunge, huku wabunge wakijuzulu katika kipindi cha siku 21 zijazo. Iwapo rais atakiuka agizo hilo, sheria yoyote ambayo itapitishwa bungeni haitakuwa na nguvu zozote," alisema Havi.
Msingi wa uamuzi wa Jaji Maranga
Jaji Maraga alisema uamuzi wake umekuja baada ya kupokea maombi kutoka kwa makundi sita ya watu ambao waliwasilisha mashtaka mahakamani.
Msingi wa maombi hayo ni maagizo kutoka kwa mahakama, ambayo yanailazimisha bunge kuunda sheria, licha ya agizo kutoka kwa mahakama ya juu mwaka 2015.
"Kuvunjwa kwa bunge kutaongeza ugumu wa uchumi pamoja na kuwa taifa lingali linakabiliana na janga la corona", alisema Jaji Maraga. Hata hivyo aliongeza kusema kuwa "hiyo ndiyo gharama ya kutekeleza katiba."
Maraga amesalia na miezi kumi kukamilisha kipindi chake cha kuhudumu kwenye kiti hicho.
Hayo yanajiri huku, tume inayosimamia uchaguzi kwa sasa ina makamishna wachache baada ya wawili kujiuzulu, jambo ambalo linaipa ugumu wa kutekeleza majukumu yake kikatiba.
Hata hivyo Spika wa Bunge la Taifa, Justin Muturi, anashikilia kuwa ni "vigumu kuutekeleza ushauri wa jaji mkuu."
Imeandikwa na Shisia Wasilwa/DW Nairobi