1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jaji Mkuu wa Kenya atoa hotuba yake ya mwisho kwa taifa

Thelma Mwadzaya27 Novemba 2020

Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga ameikamilisha rasmi safari yake ya kikazi alipolihutubia taifa kwa mara ya mwisho. Ameweka bayana kuwa hana kinyongo na Rais Uhuru Kenyatta japo walitofautiana kuhusu wajibu wa mahakama.

David Maraga Kenia
Picha: Getty Images/S.Maina

Haya yanajiri ikiwa mchakato wa kukusanya saini milioni za kuridhia mageuzi ya katiba kuanza rasmi.

Kwenye hotuba yake ya mwisho kwa taifa kama jaji mkuu wa Kenya, alipoizindua rasmi ripoti ya idara ya mahakama na uratibu wa haki, David Maraga ameweka bayana kuwa wamejitahidi kutimiza majukumu yao japo kwenye mazingira magumu ya kazi.

Kwa mtazamo wake, idara ya mahakama imekabiliana na hali ngumu kama vile kuingiliwa na pia kuvurugwa pale amri za mahakama zinapokiukwa.Hata hivyo amesisitiza kuwa hana kinyongo na Rais Uhuru Kenyatta ijapokuwa walitofautiana kwa mtazamo.

Soma pia: Jaji mkuu Kenya ataka bunge livunjwe kwa kukosekana usawa wa kijinsia

Itakumbukwa kuwa matatizo yalianza kuiandama idara baada ya mahakama ya juu kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2017 na kulazimu kurejelewa. Kufuatia kipindi hicho,Rais Uhuru Kenyatta alishikilia kuwa atalifanyia kazi suala hilo na matokeo yake yalikuwa kuipunguza bajeti ya idara ya mahakama mwaka uliofuatia wa 2018 kutokea bilioni 2.1 hadi milioni 50.

Jaji Maraga aliongoza mahakama ya juu Kenya kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2017 na kuamuru urudiwe.Picha: picture alliance/AP Photo

Kutokana na hali hiyo idara hiyo imelazimika kutimiza majukumu yake katika mazingira magumu ukizingatia kuwa upo mrundiko mkubwa wa kesi.

Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu,kesi 617,582 zinasubiria kutafutiwa suluhu.

Soma pia: Rais Kenyatta 'aishambulia' idara ya mahakama

Hata hivyo Jaji Mkuu Maraga amewapongeza majaji na mahakamu kwa kuipunguza idadi hiyo na kufikia ilipo na ana imani kuwa kesi hizo zitakamilishwa katika muda wa miaka miwili ijayo.

Kwa sasa uhusiano kati ya idara ya mahakama na serikali kuu bado haujakuwa shwari ukizingatia kuwa kibarua kilichoko ni kumsaka jaji mkuu mpya.

Maraga anastaafu katika kipindi ambacho Kenya inajiandaa kuifanyia katiba mageuzi kupitia mchakato wa maridhiano ya kitaifa wa BBI ambao unasubiri saini angalau milioni moja kuanza kufanyiwa kazi kisheria.

Jaji Mkuu David Maraga alimrithi Willy Mutunga katikati ya mwaka 2016 baada ya kustaafu miezi sita kabla muhula wake kukamilika ili kuepuka kuhusika na uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 uliogubikwa na utata.Jaji Mkuu Maraga anajiandaa kustaafu ifikapo tarehe 12 mwezi wa Januari mwakani.