1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamhuri ya Afrika kati,Algeria na Lupita Nyong'o Magazetini

7 Machi 2014

Hali jumla katika Jamhuri ya Afrika kati,Uamuzi wa Rais Abdelaziz Buteflika wa Algeria kupigania kwa mara ya nne wadhifa wa Rais na tTzo ya Oscar kwa Lupita Nyong'o ndizo Mada kuu Magazetini wiki hii.

Vikosi vya kulinda amani vya nchi za Afrika Misca vyalinda misaada ya chakula mjini BanguiPicha: DW/S. Schlindwein

Tuanzie lakini katika jamhuri ya Afrika kati ambako mhariri wa gazeti la Die Tageszeitung,Simone Schlindwein alifika mji mkuu Bangui na kuelekea pia kaskazini katika mji wa Sibut inakopitia njia kuelekea Tchad pakiwepo uwezekano wa kufika Libya na hata katika bahari ya kati. Njia hiyo ndiyo iliyotumiwa mwaka mmoja uliopita na waasi wa Seleka kuingia madarakani mjini Bangui.Hivi sasa lakini anasema Simone Schwindlein,humuoni hata muumini mmoja wa kiislam,wote wametimuliwa na eneo hilo kudhibitiwa na wanamgambo wenye mapanga na marungu.Kilomita 13 kutoka Bangui ndiko balaa linakokutikana anasema na kuelezea jinsi waumini kama elfu moja hivi wa kiislam wanavyoishi nje,kwenye vibanda vya mabati,misikitini,si mbali na mahala wanakokutikana wanamgambo wa Anti Balaka ambao miezi iliyopita waliwauwa waislam na kuwakata vipande vipande,wengine wamewatia moto wahai na kufika hadi ya kula nyama zao.

Wanamgambo wanajiandaa msituni

Ingawa vikosi vya Ufaransa vinapiga doria na kulinda ujia wa kati ya kilomita 12 na 13 lakini baada ya hapo hakuna anayedhamini usalama - hilo ni eneo lisilokuwa na wenyewe anasema ripota wa die Tageszeitung Simone Schlindwein.Na kuanzia hapo hadi kufikia umbali wa kilomita 120 ndiko wanamgambo wa Anti Balaka na marungu na mapanga yao wanakozuwia magari, na kulazimisha wapatiwe vitu mfano wa sigara na pesa. Ni vijana, wengine ni watoto, wenye wasi wasi na wasiogopa kitu. Vijiji vya karibu na fukwe vimeachwa vitupu.Sibut umbali wa kilomita 180 kaskazini ya mji mkuu Bangui hali inatisha anasema ripota wa die Tageszeitung,kwa sababu si mbali na huko wanamgambo wa Seleka wamejificha misituni, wanajiandaa kulipiza kisasi. Katika ripoti nyengine die Tageszeitung linazungumzia wito wa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon wa kutumwa wanajeshi 12 000 na polisi katika nchi hiyo na kusema wanajeshi wa kikosi cha kulinda amani cha nchi za Afrika Micra na wale wa Ufaransa hawatoshi.

Wakimbizi wa kislam wamekimbilia katika auwanja wa kanisa huko BoaliPicha: Bettina Rühl

Ujerumani yaaghidi kusaidia

Na hatimaye katika mada hiyo hiyo ya Afrika kati, gazeti la mji mkuu Berliner Zeitung linazungumzia mchango wa Ujerumani katika juhudi za kurejesha amani katika jamhuri ya Afrika Kati. Serikali kuu ya Ujerumani imependekeza kutuma madege yake chapa Medivac ambayo ni aina ya hospitali ya angani inayowapatia matibabu majeruhi na kuwapeleka katika hospitali za Ulaya. Ujerumani inafikiria pia uwezekano wa kutuma washauri wa kijeshi katika makao makuu ya jeshi la Ulaya nchini Ugiriki na katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya kati Bangui."Ni chini ya maafisa 20 limesema Berliner Zeitung lililomnukuu msemaji wa masuala ya ulinzi wa chama cha SPD Rainer Arnold. Hawatoshiriki katika mapigano, hilo limekataliwa tangu mwanzo na waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen, limemaliza kuandika gazeti la Berliner Zeitung.

Bouteflika habanduki madarakani Algeria

Gazeti la die Tageszeitung limeandika kuhusu uamuzi wa rais wa Algeria Abdel Aziz Bouteflika, mwenye umri wa miaka 77 kupigania mhula wa nne uchaguzi wa rais utakapoitishwa Aprili 17 ijayo. "Atashinda "linaandika gazeti hilo likihoji taasisi zote za serikali, vyama vyote vilivyoko madarakani na jeshi wanamuunga mkono. Zaidi ya hayo linaandika die Tageszeitung, kati ya wagombea wepya wa upande wa upinzani hakuna yeyote anayejivunia umaarufu nchini humo.Wafuasi wa itikadi kali wameamua kutopigania wadhifa wa rais na vuguvugu la jamii kwa ajili ya amani MSP pamoja na chama cha Machipuko Ennahda vimeamua kuususia uchaguzi huo. Baadhi ya wananchi akiwemo amiri jeshi wa zamani Mohand Tahar Yalatat wanazungumzia kuhusu "kundi la mafia lililoiteka nyara Algeria. Wanataka utaratibu wa kupiga kura usitishwe, pawepo miaka miwili ya kipindi cha mpito kuelekea demokrasia halisi. Hata vyombo vya habari vya Algeria vinajiuliza ni daktari gani huyo aliyempatia Bouteflika cheti kinachothibitisha anaweza kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi chengine cha miaka mitano. Die Tageszeitung linakumbusha Bouteflika alipowasilisha maombi ya kugombea wadhifa wa rais, picha kidogo tu ndizo zilizonyeshwa katika tekevisheni na sauti yake haijasikika.

Maandamano dhidi ya serikali ya AlgeriaPicha: FAROUK BATICHE/AFP/Getty Images

Msanii mrembo wa Kenya atunukiwa Oscar

Na hatimaye lilikuwa gazeti la Süddeutsche Zeitung lililozungumzia fahari ya Kenya na Afrika kwa jumla kwa kutunukiwa tuzo ya Oscar mchezaji sinema Lupita Nyong'o kama mchezaji sinema bora katika filamu iliyopewa jina "12 Years a Slave"-"Mtumwa kwa miaka 12."Ilikuwa filamu yake ya kwanza katika ulimwengu wa Hollywood anakumbusha ripota wa Süddeutsche Zeitung.

Lupita Nyong'o akitoa shukurani zake baada ya kutunukiwa Oscar huko Hollywood CaliforniaPicha: Reuters

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL PRESSE

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW