Jamhuri ya Afrika ya Kati yaudhibiti mji kutoka kwa waasi
4 Februari 2021Vikosi tiifu kwa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati vimeudhibiti tena mji muhimu kutoka mikononi mwa waasi, wakati wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakiendelea kuimarisha udhibiti. Waziri mkuu wa taifa hilo Firmin Ngrebada, amesema wanajeshi wa serikali na washirika wao wameudhibiti mji wa Bossembele, ulioko kilometa 150 kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Bangui. Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imekuwa ikisaidiwa na vikosi vya Rwanda na wanajeshi wa Urusi. Bossembele ulikuwa moja wapo ya miji muhimu iliotumiwa na vikundi vya waasi walio na silaha katika mashambulizi yaliyoanzishwa dhidi ya mji mkuu Bangui mnamo Desemba, wakati walipoungana chini ya mwamvuli wa Coalition of Patriots for Change (CPC) kujaribu kuzuia kuchaguliwa tena kwa Rais Faustin Archange Touadera. Miaka nane ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, waasi wanashikilia karibu theluthi mbili ya maeneo ya taifa hilo.