1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC kufanya uchaguzi mkuu Desemba 2023

Daniel Gakuba
26 Novemba 2022

Tume ya taifa ya uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema uchaguzi mkuu nchini humo utafanyika Desemba 20, 2023, licha ya kuzorota kwa usalama mashariki mwa nchi hiyo.

Wahlen in Kongo 28.11.2011
Picha: picture-alliance/dpa

Tangazo la tume hiyo, CENI lililotolewa Jumamosi limekuja wakati waasi wakiendeleza harakati zao katika mkoa wa Kivu Kaskazini, katika ghasia ambazo zimewalazimisha makumi kwa maelfu ya raia kuyakimbia makaazi yao.

Hata hivyo, rais wa tume hiyo ameonya akisema ''kuendelea kwa matatizo ya kiusalama katika baadhi ya maeneo'' kutakuwa changamoto katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa '' huru, wazi na wa haki.''

Soma zaidi: DRC na Rwanda zapata mwafaka kuhusu vita mashariki mwa DRC

Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, chaguzi za rais, wabunge na serikali za mitaa hufanyika kwa wakati mmoja. Kulingana na katib ya nchi hiyo, rais mteule atachukua madaraka mwezi Januari 2024.

Felix Tshisekedi, rais wa DRCPicha: Philbert Rweyemamu/EAC

Mara ya kwanza kubadilishana madaraka kwa amani

Rais wa sasa, Felix Tshisekedi aliingia ofisini Januari 2019, akirithi kiti kilichoachwa wazi na mtangulizi wake, Joseph Kabila aliyeongoza kwa miaka 18 iliyotawaliwa na misukosuko.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa rais mmoja kukabidhi mamlaka kwa rais mwingine kwa njia ya amani katika historia ya nchi hiyo.

Licha ya utata ulioghubika kuchaguliwa kwake kuongoza muhula wa kwanza, Tshisekedi amekwishabainisha azma yake ya kugombea tena.

Soma zaidi: Tume ya uchaguzi Congo yatangaza ratiba ya uchaguzi mkuu

Watu wengine wanaotarajia kujitosa katika kinyang'anyiro hicho ni Martin Fayulu aliyetangazwa kuwa mshindi wa pili katika uchaguzi wa mwaka 2018, ingawa yeye anashikilia kuwa alipokonywa ushindi.

Wanasiasa wengine wanaoaminika kuwa na ndoto ya kugombea, kama waziri mkuu wa zamani Adolphe Muzito, na aliyekuwa gavana wa jimbo la Katanga, Moise Katumbi, bado hawajajitokeza kutangaza nia yao hadharani.

Rais wa zamani wa DRC, Joseph KabilaPicha: AP

Matata Ponyo naye kurusha karata yake

Mtu mwingine ambaye tayari amesema atagombea urais ni Augustin Matata Ponyo, ambaye pia aliwahi kushikilia wadhifa wa waziri mkuu. Mwaka uliopita, Ponyo alishitakiwa kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali ya umma, lakini Mahakama ya Katiba ilijiondoa katika kesi yake ikisema haina uwezo kisheria kumhukumu.

Soma zaidi: DRC: Waziri mkuu wa zamani Matata Ponyo aachiwa huru 

Hata hivyo, majaji wa mahakama hiyo sasa wamebadilisha, na sasa inasema inaweza kurejea katika kesi dhidi yake.

Kutawazwa kwa Felix Tshisekedi mwaka 2019 kulihitimisha miaka miwili ya sintofahamu, iliyosababishwa na hatua ya Joseph Kabila kugoma kuachia madaraka baada ya muhula wake wa mwisho kumalizika.

Chaguzi mbili ambamo Kabila alitangazwa mshindi ziliambatana na umwagaji wa damu. Watu dazeni kadhaa waliuawa katika maandamano yaliyoripuka kufuatia uamuzi wa Kabila kung'ang'ania kiti baada ya muda wake kumalizika.

 

Chanzo: AFPE

 

   

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW