Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yaingia kwenye mgogoro
10 Desemba 2011Baada ya tume ya uchaguzi kusema kwamba Kabila ameshinda uchaguzi huo wa rais uliofanyika Novemba 28 kwa asilimia 49 ya kura zote dhidi ya Tshisekedi aliyejinyakulia asilimia 32 ya kura, maandamano yaliyogubikwa na ghasia yalizuka katika miji mbali mbali iliyoko nje ya mji mkuu Kinshasa.Waandamanaji isasi angani.
Uporaji pia umeripotiwa kutokea katika miji kadhaa nje ya Kinshasa huku alau mtu mmoja akijeruhiwa baada ya kupigwa risasi. Kwa muda wa wiki nzima usalama umeimarishwa ambapo polisi na walinzi wa rais wamekuwa wakipiga diria pamoja na wanajeshi 20,000 waliokuwa wamejiweka tayari waliyazima maandamano na kuyazuia kusambaa.
Hakujakuweko na ghasia kubwa usiku wa kuamkia leo na hali katika mji mkuu asubuhi ya leo imeonekana kuwa shwari. Jana ijumaa katikati ya mji wa Kananga ambako ni ngome ya kambi ya Tshisekedi vurugu zilizuka lakini zilizimwa na polisi kama ilivyotokea mjini Kinshasa.
Wadadisi wa amambo walionya kwamba uchaguzi huo mkuu nchini Kongo ambao ni wa pili tangu kumalizika vita vilivyofuatana vya mwaka 1996 hadi 2003 unatishia kuzusha ghasia mpya katika nchi hiyo kubwa ya Afrika ya kati.
Itakumbukwa kwamba kampeini za uchaguzi huo pia zilitawaliwa na umwagikaji wa damu ambapo kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kiasi ya raia 18 waliuliwa wengi wao ikiwa ni kutokana na kupigwa risasi na walinzi wa rais Kabila.
Kongo bado iko katika hali ya wasiwasi na kutofahamika nini kitatokea baadae. Ijumaa Tshisekedi aliyataja matokeo ya uchaguzi kuwa ni uchokozi dhidi ya watu wake na amekataa kukata rufaa kuyapinga matokeo hayo kisheria. Kimsingi mahakama kuu inajukumu la kuyatathmini matokeo, kusikiliza mivutano kuhusu uchaguzi huo na kumtangaza mshindi halali hapo Disemba 17.
Hata hivyo kuna wasiwasi juu ya uhuru wa Mahakama hiyo baada ya maofisa wake kuongezwa kutoka 7 hadi 27 katika kipindi cha mwanzo wa kampeini za uchaguzi.
Mgombea wa Upinzani, Etienne Tshisekedi, anasema mahakama hiyo ni taasisi ya kibinafsi ya Kabila na ndio sababu chama chake hakiwezi kupeleka rufaa mbele ya majaji wa mahakama hiyo. Tshisekedi anadai ameshinda uchaguzi kwa asilimia 54 akifuatiwa na Kabila aliyepata asilimia 26.
Kutokana na hesabu hiyo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba anajitambua tangu sasa kuwa rais mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mgombea aliyeko katika nafasi ya tatu Vital Kamerhe pia ameyapinga matokeo rasmi na kusema kwamba anamtambua Tshisekedi kama rais mpya. Jumuiya ya Kimataifa kwa kauli moja imewataka Wakongo wakiwemo wanasiasa wawe watulivu.
Mwandishi: Saumu Mwasimba/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef